Kamati ya Maadili CCM yakutana; Ilichojadili ni Siri, siri, Siri!

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKATI mbambo si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kamati ya Maadili jana imekutana kwenye kikao cha siri Makao Makuu ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete kujadili masuala kadhaa.

Vyanzo vya habari vya mtandao huu vinabainisha kuwa Kikwete aliwasili makao makuu kwenye vikao hivyo saa tano ambapo aliendelea na vikao na viongozi wenzake, ikiwa ni siku moja kabla ya vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC).

Taarifa ambazo dev.kisakuzi.com imezipata CC itakutana kesho na baadaye kufuatiwa na kikao cha NEC kitakachofanyika Novemba 23 hadi 24 Mwaka 2011. Taarifa zaidi zinasema Kamati ya maadili imewaweka kiti moto baadhi ya vigogo wakiwemo viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM ambao wamekuwa wakikigawa chama dhidi ya kauli tata ambazo zimekuwa zikiibuka.

Habari ambazo hazikuweza kuthibitishwa zinadai Kamati hiyo pia imejadili falsafa ya kujivua gamba na utekelezwaji wake, kwa vigogo wenye tuhuma ambao hadi leo wamezindwa kujivua gamba kwa hiyari yao.

“Wanajadili falsafa nzima ya kujivua gamba na utekelezaji wake…maana kuna vigogo wenye tuhuma wanaonekana kugoma kufanya hivyo kwa hiyari yao, sasa wataangalia nini cha kufanya ili kukinusuru chama na maswala mengine ikiwa ni maandalizi ya ajenda za mkutano unaofuata,” kimesema chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya CCM.

Hata hivyo akizungumza na wanahabari jana jioni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati alisema Kamati ya Maadili ni sehemu ya CC na wamekutana kuandaa ajenda za mkutano uliokuwa ukifuatia (leo).

Kiongozi huyo aligoma kuweka wazi kama kunabaadhi ya vigogo walihojiwa kwenye vikao vya Kamati ya Maadili na kusisitiza wanahabari kuwa na subira, kupata taarifa baada ya Vikao vya NEC.