Kamati ya Kuzuia Ukatili kwa Wanawake yazinduliwa Tanzania

Vipigo kwa wanawake nao ni unyanyasaji wa kundi hilo.

Na Mwandishi Wetu

KAMATI Maalumu itakayofanya kazi ya kuzuia vitendo vya kikatili kwa Wanawake nchini Tanzania imezinduliwa jijini Dar es Salaam. Kamati hiyo ya Kitaifa imezinduliwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe.

Akizungumza katika uzinduzi wa kamati hiyo, Maembe alisema licha ya uwepo wa kauli za kupinga vitendo vya unyanyasaji kama, Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004, Mkataba wa Ulinzi, Amani na Maendeleo ya Mtoto wa mwaka 2006, Tanzania bado imekuwa na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake hasa vile vya ukeketaji, ubakaji, unyanyasaji na vipigo.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameitaja mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kuwa ni pamoja na Mkoa wa Mara, Manyara, Kilimanjaro na Mkoa wa Dodoma.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Meshack Ndaskoi alisema Kamati hiyo sasa itafuatilia utekelezaji wa Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004 na makubaliano ya nchi za maziwa makuu. Tanzania bado inaongoza kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, na hata ukatili wa watoto na walemavu wa ngozi albino.