Kamati TFF Yatupa Rufani ya Timu ya Mwanza Wanawake
KAMATI ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetupa rufani ya timu ya Mwanza kupinga uhalali wa wachezaji wawili wa Kigoma kwenye mechi yao ya robo fainali iliyochezwa jana (Januari 26 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mwanza iliyopoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1 iliwalalamikia wachezaji Neema Sanga na Vene Dickson wa Kigoma kuwa waliwahi kuchezea timu ya Taifa (Twiga Stars), hivyo kucheza mashindano ya Kombe la Taifa la Wanawake ni kinyume cha kanuni.
Kamati baada ya kupitia rufani hiyo, imeitupa kwa vile timu ya Mwanza haikuwasilisha vielelezo vyovyote kuthibitisha madai hayo dhidi ya wachezaji hao. Pia Kamati yenyewe ilipitia taarifa za Twiga Stars ambapo haikupata kumbukumbu za wachezaji hao katika timu hiyo.
Pia Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kugomea uamuzi dhidi ya rufani yao, hivyo imependekeza Mwenyekiti wa TWFA Mwanza, Sophia Tigalyoma na Katibu wake Hawa Bajanguo wapelekwe Kamati ya Nidhamu kwa hatua za kinidhamu.
WASHINDI COPA COCA-COLA WAKABIDHIWA VITITA VYAO
Washindi wa Copa Coca-Cola 2014 wamekabidhiwa zawadi zao za fedha kutoka kwa mdhamini wa michuano hiyo ya umri chini ya miaka 15 kwa wavulana na wasichana kampuni ya Coca-Cola. Fedha hizo kwa washindi mbalimbali tayari zimeingizwa kwenye akaunti zao.
Kwa upande wa wavulana; washindi na kiwango walichopata ni mabingwa Dodoma (sh. milioni nane), makamu bingwa Kinondoni (sh. milioni tano), mshindi wa tatu Kigoma (sh. milioni tatu) wakati timu yenye nidhamu Tanga (sh. milioni moja).
Mchezaji bora Mwami Ismail kutoka Kigoma (sh. 500,000), mfungaji bora Timoth Timoth wa Dodoma (sh. 500,000), kipa bora Kelvin Deogratia wa Geita (sh. 500,000) na mwamuzi bora Abdallah Mbarome kutoka Zanzibar sh. 500,000).
Kwa upande wa wasichana ni mabingwa Kinondoni (sh. milioni tano), makamu bingwa Ilala (sh. milioni tatu), mshindi wa watatu Temeke (sh. milioni mbili) wakati timu yenye nidhamu Mbeya imepata sh. milioni moja).
Zubeda Mohamed wa Kinondoni ambaye ndiye mchezaji bora amepata sh. 500,000, mfungaji bora Stumai Abdallah wa Temeke sh. 500,000 wakati kipa bora ni Suleta Saad wa Zanzibar sh. 500,000.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)