KAMATI ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Agosti 10 na 11 mwaka huu kujadili rufani ya Frank Mchaki kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kumuengua kugombea nafasi ya Katibu Mkuu katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA).
Chini ya Mwenyekiti wake Deogratias Lyatto, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa pingamizi lililowekwa dhidi ya Mchaki na kujadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, liliwasilishwa, kujadiliwa na kutolewa uamuzi kinyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 11(2) na (3) kwa kutotanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya KIFA, hivyo rufani hiyo haikuwa na sifa ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Hata hivyo baada ya kupitia kiini cha pingamizi, Kamati imefikia uamuzi kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya mrufani zimekosa ithibati.
Kutokana na maelezo hayo, Kamati imekubaliana na rufani ya mrufani (Mchaki) dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, hivyo imemrejesha kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa KIFA.
Kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 8(3) Kamati ya Uchaguzi ya TFF inauahirisha uchaguzi wa KIFA uliokuwa ufanyike Agosti 13 mwaka huu na sasa utafanyika Agosti 20 mwaka huu.