Janeth Mushi, Arusha
KATIKA hali isiokuwa ya kawaida Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa leo amewatimuwa waandishi wa habari waliokuwa nje ya Ofisi Kuu ya Jeshi hilo mkoani Arusha.
Kaimu huyo alifikia hatua hiyo jana mchana wakati waandishi walipokuwa wakisubiri hatma ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani hapa, James Ole Millya.
Aidha Millya ambaye juzi alijisalimisha katika Jeshi la Polisi baada
ya polisi kudai kuwa wanamtafuta kwa mahojiano ili aweze kuthibitisha
kauli anazodaiwa kuzitoa katika Mkutano wa kufungua matawi Mjini
hapa,ambazo zimelidhalilisha Jeshi hilo.
Mpwapwa “aliwatimua” wanahabari kwa madai kuwa muda wa kuonana nao umeshapita (saa 5 asubuhi) ambapo alipoelezwa kuwa wanasubiri kujua hatma ya Millya ambaye alikuwa afike saa 8 katika makao makuu hayo kwa ajili ya mahojiano.
“Huu siyo muda wa kuchukua habari nakutanaga na nyie saa 5 hivyo
tokeni mkachukue habari huko mtaani, sina muda wa kukutana na ninyi
waandishi saa hizi,” alidai Mpwapwa
Kufuatia hali hiyo waandishi wa habari mkoani hapa, wamegoma kufuatilia na kuandika habari za Polisi hadi hapo Kamanda huyo atakapoomba radhi kwa kuwa amewadhalilisha.
“Ifike wakati taaluma ya habari iheshimiwe kama taaluma nyingine hapa
nchini kwani kwa kitendo hiki Kaimu ametudhalilisha na kutudharau, kwani lengo letu kuwa hapa ni kumsubiri Millya ahojiwe ili tuweze kuzungumza nae,” alisema mmoja wa waandishi ambaye hakutaka jina
lake lichapishwe gazetini
Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM akizungumza na waandishi wa habari nje ya makao makuu ya Jeshi hilo baada ya kuhojiwa kuanzia na Mkuu wa Upelelezi mkoani hapa, saa 8;40 hadi 9;55 mchana alisema kuwa kwa sasa hawezi kuongea chochote kuhusiana na alichokijadili na ofisa huyo wa polisi, kwa kuwa hizo ni siri kubwa. Mwenyekiti huyo aliwataka Watanzania kuamka na kupigania haki yao na kuwa kupigania haki siyo kuvunja sheria.
“Haki hailetwi kwenye sahanai na badala yake inapiganiwa na mimi
ninajua nina haki baada ya mambo haya kukamilika tutazungumza chanzo cha mambo haya na kujua ukweli kwani mimi najua napigania
haki,” aliwaeleza waandishi.