Kafulila, wenzake hawajapewa barua kuvuliwa uanachama NCCR

Mh. David Kafulila

UONGOZI wa NCCR-Mageuzi umeshikwa ghafla na kigugumizi baada ya hadi sasa kushindwa kumpa barua Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, na wenzake watatu, kuthibitisha uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) wa kuvuliwa kwao uanachama wa chama hicho.

Wengine ambao hadi kufikia jana uongozi wa NCCR-Mageuzi ulikuwa bado haujawapa barua za kuthibitisha uamuzi wa NEC, ni wanachama 19 wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali, waliopewa karipio kali na NEC.

Kafulila na wenzake hao, akiwamo aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Hashim Rungwe.

Wengine ni aliyekuwa Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan na Yothamu Lubungira, walitangazwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samwel Ruhuza, kwamba wamevuliwa uanachama na NEC.

Kafulila, wenzake waliovuliwa uanachama na wanachama waliopewa karipio kali, walichukuliwa hatua hiyo kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kutokana na kujihusisha na mgogoro ndani ya chama hicho.

Ruhuza alipoulizwa na NIPASHE jana kama tayari uongozi wa NCCR-Mageuzi umekwisha kupeleka barua kwa Spika wa Bunge kumuarifu kuhusu uamuzi wa NEC uliochukuliwa dhidi ya Kafulila, alijibu kwa kifupi kwamba “bado tunaendelea na utaratibu.”

CHANZO: NIPASHE