Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila, amesema yuko tayari kukihama chama chake na kujiunga na chama kingine ikiwa atashindwa kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama aliyoifungua mahakamani.
Kafulila aliyasema hayo wakati akizungumza na NIPASHE jijini Mbeya na kuwa ana uhakika wa kushinda kiti cha ubunge kwenye jimbo lake hata kama atagombea kupitia chama kingine, hivyo uamuzi wa kutimuliwa NCCR Mageuzi hamuumizi kichwa.
Alisema kuwa endapo mahakama itaamua kubariki uamuzi wa yeye kufukuzwa NCCR Mageuzi, hana mpango wa kukata rufaa katika Mahakama ya juu, badala yake atahamia chama kingine na kurudi jimboni kuomba ridhaa ya wananchi aendelee kuwa mbunge wao.
Hata hivyo Kafulila hakuwa tayari kutaja chama anachokusudia kuhamia, akisema kuwa hilo atalisema baada ya mahakama kutoa uamuzi wa kesi aliyoifungua mahakamani.
“Nimesema nitahamia chama chochote, tusubiri uamuzi wa mahakama kama utaniondoa NCCR Mageuzi ndipo nitakuwa tayari kutamka chama gani najiunga nacho,” alisema Kafulila. Kafulila alijiunga na NCCR Mageuzi mwaka 2010 akitokea Chadema.
Hata hivyo mwaka jana alihitlafiana na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia hali iliyosababishwa avuliwe uanachama kabla ya kukimbilia mahakamani.
CHANZO: NIPASHE