Hatima ya ubunge wa David Kafulila aliyetangazwa kuvuliwa uanachama wa NCCR-Mageuzi na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, hadi sasa bado kitendawili. Hali hiyo imedhihirika baada ya Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza, kueleza wamekwisha kuliarifu Bunge kuhusu uamuzi huo wa NEC dhidi ya Kafulila, huku Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, akisema bado hajaiona taarifa yoyote ya chama hicho.
Ruhuza alilieleza NIPASHE jana kuwa barua ya kuliarifu Bunge kuhusu uamuzi huo wa NEC dhidi ya Kafulila alikabidhiwa mmoja wa maafisa wa NCCR-Mageuzi kuipeleka bungeni jana. Hata hivyo, alisema hajui kama afisa huyo wa NCCR-Mageuzi aliipeleka barua hiyo katika ofisi za Bunge au la. Afisa huyo wa NCCR-Mageuzi hajajulikana na wala Ruhuza hakuwa tayari jana kumtaja. Badala yake, Ruhuza mara zote alipokuwa akihojiwa na NIPASHE alikuwa akisisitiza kumtaka mwandishi awasiliane na Katibu wa Bunge.
“Muulize Katibu wa Bunge. Akikwambia wameipata, basi andika tumepeleka. Akikwambia hajaipata, andika hatujapaleka,” alisema Ruhuza. Kutokana na hali hiyo, NIPASHE iliwasiliana na Dk. Kashililah, ambaye alisema kufikia jana jioni, hakukuwa na barua yoyote ya NCCR-Mageuzi iliyopelekwa ofisini kwake. “Sijui watakuwa wameipeleka kwa nani,” alisema Dk. Kashililah.