Kafulila apewa siku 14 za kukata rufaa

Mbunge wa Kigoma Kusini, Mh. David Kafulila

Licha ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, na wenzake watatu, chama hicho kimewapa siku 14 za kukata rufaa kwenye Mkutano Mkuu kupinga uamuzi huo dhidi yao, huku kikimpa Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali, karipio kali kutokana na kujihusisha na mgogoro katika chama.

Wakati NCCR-Mageuzi ikitangaza hayo, Kafulila jana aliibuka na kuzungumzia kumwaga kwake machozi, huku akisisitiza kuwa ufumbuzi juu ya uamuzi uliochukuliwa na NEC dhidi yake na wenzake, utapatikana kwa njia za mazungumzo au sheria za nchi.

Na katika hatua za awali, habari zinasema kuwa jana asubuhi, Kafulila alifanya kikao na baadhi ya wazee wa NCCR-Mageuzi, katika ofisi za chama hicho.

Wengine waliovuliwa uanachama pamoja na Kafulila, ni pamoja na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Hashim Rungwe, aliyekuwa Kamishna wa Chama hicho Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan na Yothamu Lubungira.

Iwapo Spika wa Bunge atabariki uamuzi huo wa NEC-NCCR-Mageuzi dhidi ya Kafulila, atakuwa amepoteza sifa za kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi wa kuvuliwa uanachama Kafulila na wenzake hao ulichukuliwana NEC-NCCR-Mageuzi, katika kikao chake kilichofanyika Desemba 17, mwaka huu.

KAULI YA KATIBU MKUU

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa uamuzi huo ulifikiwa na NEC ikiwa ni chombo kikuu cha nidhamu cha Taifa na kwa mujibu wa Ibara ya 5 (9), ya kanuni za nidhamu na usuluhishi za chama za mwaka 2002.

“Baada ya hoja ya kwanza, kikao kilijadili tuhuma dhidi ya David Kafulila na wanachama wengine ambao walijenga mtafuruku ndani ya chama kwa kukipiga vita chama nje ya vikao vya chama, Halmashauri Kuu iliwaona wana makosa, na baada ya hapo wajumbe waliamua kumvua uanachama David Kafulila,” alisema Ruhuza.

Alisema kikao hicho kilijadili na kupokea utetezi wa Mwenyekiti Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kutokana na tuhuma zilizowasilishwa na aliyekuwa Mbwana pamoja na wanachama wengine 26, waliosaini hati ya kutokuwa na imani naye (Mbatia).

Ruhuza alisema pamoja na tuhuma hizo, wajumbe hao wa NEC walimuona Mbatia hana tuhuma za kujibu na kuzitupilia mbali na kutoa maazimio matatu.

“Halmashauri Kuu ilimpa pole na pongezi Mwenyekiti wa Taifa kwa kuvumilia tuhuma zisizo na msingi dhidi yake na Chama hakitavumilia kuona wanachama au viongozi wanakuwa watovu wa nidhamu na hasa kuleta migogoro yenye mwelekeo wa kikibomoa au kukidhoofisha chama,” alisema Ruhuza.

“Hivyo Halmashauri Kuu, ilimuona Mbatia kuwa kiongozi safi, hodari na shujaa wa chama,” aliongeza.

Alisema kikao hicho cha NEC, kiliwavua pia uongozi Lucy Kapia, Ali Omar Juma na James Baztisa, huku wengine 19 wakipewa karipio kali, akiwamo Mkosamali.

WALIOKARIPIWA

Wengine waliopewa karipio kali, aliwataja kuwa ni Joseph Antony Nyoni, Issa Abass Hussen, Ameir Mshindani Ali, Kayumbo Kabutali, Bashiry Bayona, Daimon Mwamsampeta, Kassim Libenanga, Patrick Salhanga, Greyson Mwasenga na Amina Suleiman.

Wamo pia Juma Abdallah Vuai, Maryam Salehe Juma, Suwed Othman, Salma Mohamed Juma na Henry Mapunda.

Ruhuza alisema katika kutoa adhabu kwa waliopatikana na makosa, NEC iliangalia umuhimu wa kumaliza migogoro kwa amani na iliwasamehe wanachama wote walioamua kujitoa kwenye mgogoro mapema kabla ya kuomba radhi walipopewa fursa ya kujitetea mbele ya kikao.

WABUNGE WA KASULU WAZUNGUMZA

Mbunge wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Zaituni Buyogera, alisema mara baada ya Kafulila kuhamia NCCR-Mageuzi, alikabidhiwa kutembea naye vijiji vyote vya Jimbo la Kigoma Kusini, ili kumtambulisha kwa wanachama na wananchi.

“Mimi ni mzazi, na ninaujua uchungu wa kujifungua na unapokuwa na mtoto, ambaye kila siku unamkanya lakini hakusikii basi unawaachia walimwengu ili wahukumu na ndicho kilichotokea kwa huyo kijana wangu Kafulila,” alisema.

Aliongeza: “Najua roho inauma ila sina budi na ninasikitika kwa hili lilotokea dhidi yake na lipo nje ya uwezo wangu.”

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema hatua ya kutopatikana ufanisi katika idara za umma, vikiwamo vyama vya siasa ni kukosekana nidhamu kwa kushindwa kufuata kanuni, taratibu na sheria kama ilivyotokea kwa mbunge wenzake.

“Ni mara nyingi nilikuwa nikimsihi asifanye haya mambo nje ya vikao. Na katika kikao kilichopita tuliweka azimio la kutokutoa taarifa nje ya vikao. Siku ya pili naona katika vyombo vya habari, tena vikimnukuu ndugu yangu Kafulila. Sasa acha sheria ichukue mkondo wake,” alisema Machali.

KATIBU WA BUNGE: DEMOKRASIA IFUATWE

Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema jana kuwa uamuzi wa NEC dhidi ya Kafulila, utakubaliwa na Bunge iwapo demokrasia katika kufikia uamuzi huo ilizingatiwa.

Dk. Kashililah alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE kueleza vigezo vinavyotumiwa na Bunge kukubali uamuzi unaofikiwa na chama cha siasa kumvua uanachama mbunge.

“Inategemea watakavyotuandikia. Si unakumbuka mwaka ule NCCR walivyopeleka kwa Spika taarifa za kuwavua uanachama Marando na Chiku Abwao, lakini Spika akakataa kutokana na kikao kilichowavua kuwa na matatizo? Sasa kikao kitaangaliwa, pia sababu zitaangaliwa. Kwa sababu hii ni nchi ya demokrasia. Hivyo, lazima demokrasia iangaliwe,” alisema Dk. Kashililah.

KAULI YA KAFULILA

Naye Kafulila akizungumzia kutokwa na machozi baada ya kuvuliwa uanachama, alisema hali hiyo ilimtokea baada ya kuwakumbuka wananchi wa jimboni kwake.

“Nilitokwa na machozi baada ya kuwakumbuka wananchi wa Kigoma Kusini. Nimefanya mengi na nina mipango mingi ya kusaidia wananchi wa Kigoma katika nyanja mbalimbali. Ufumbuzi wa tatizo hili utapatikana kwa njia ya mazungumzo au sheria za nchi,” alisema Kafulila kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) alioutuma kwa mwandishi wa habari hii jana.

Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni jana, kilichojiri katika mazungumzo kati ya Kafulila na wazee wa NCCR-Mageuzi, hakikuweza kufahamika.

JK kukutana na NCCR, NGO’s

Wakati huo huo, Chama cha NCCR- Mageuzi kimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa nia ya kutoa mawazo yake kuhusu mchakato wa kutungwa kwa Katibu Mpya ya Tanzania, kama ilivyoahidiwa kwa wananchi na Rais mwenyewe mwishoni mwa mwaka jana.

Aidha, Baraza la Taifa la Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s) limeomba kukutana na kuzungumza na Rais kuhusu mchakato huo huo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilieleza jana kuwa, Rais Kikwete ameyakubali maombi yote mawili na ameagiza wahusika kupanga mikutano hiyo kati yake na Chama cha NNCR-Mageuzi na kati yake na Baraza la Taifa la NGO’s.

Tayari Rais amekutana na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chdema) na ule wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu mchakato huo baada ya kuwa ameomba kukutana na viongozi wa vyama hivyo.

Mikutano kati ya Rais na viongozi wa vyama hivyo ilimalizika kwa maridhiano na maelewano juu ya namna bora zaidi ya kusukuma mchakato huo kwa namna inavyofaa kwa mustakabali wa nchi.

CHANZO: NIPASHE