Kafulila ‘achafua’ hewa bungeni


Bungeni Dodoma.

*Sitta awabeza wapinzani, awaita wanafiki

Dodoma

HALI ya hewa bungeni imechafuka baada ya ukumbi kugeuka sehemu ya zogo, ambapo wabunge wametoleana lugha za kubezana na kuzomeana kama watoto.
Hatua hiyo imeibuka Bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR- Mageuzi), kunukuu kauli aliyoiita ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa ‘Serikali legelege’ haiwezi kukusanya kodi.

Kafulila alitoa kauli hiyo, wakati akichangia hotuba ya, Makadirio, Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka 2011/2012 ya Wazara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyowasilishwa juzi na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hadji Mponda.

Katika mchango wake, Kafulila alisema Serikali imekosa dhamira ya kweli ya kuboresha afya za wananchi na kuongeza kuwa “sisi ndiyo tuna uwiano mbovu kati ya madaktari na wagonjwa…Sisi tunategemea wafadhiri kutupa fedha za sekta ya afya hii ni aibu. Fedha zilizotengwa ni kidogo sana, yaani tunategemea fedha kutoka nje halafu za ndani mnatenga kiasi kidogo namna hii.
….Fedha zipo mnashindwa kutoza kodi. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Serikali legelege haitozi kodi,” alisema Kafulila.
Baada ya kusema hivyo ndipo Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla (CCM), aliposimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti akimtaka Kafulila afute kauli yake kwamba ‘serikali legelege’ haikusanyi kodi na kwamba kauli hiyo ni ya kuudhi.
Dk. Kigwangalla alisema Serikali ya CCM siyo legelege kwani imekuwa ikikusanya kodi na hivyo kuliingizia taifa mapato ya kutosha.
Hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama akampa fursa, Kafulila afute kauli yake lakini mbunge huyo alisema “mimi nimenukuu kauli ya Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa hili ambaye wote tunamuenzi bila kuzingatia itikadi za vyama vyetu”
“Nasikitika tunatumia muda mwingi kujadili jambo hili. Nilichosema ni nukuu na niko tayari kuifia,” alisema Kafulila.
Sitta awabeza wapinzani
Hali ilichafua zaidi baada ya Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali, Samuel Sitta kusimama na kusema kuwa “mimi ningewashauri wabunge wenzangu wa CCM, wapinzani kazi yao ndiyo hiyo kukosoa kila kitu serikali inachofanya.
…Wana lugha nyepesi, mambo yao yamekaa kwenye unafiki. Baadhi yao wanasema eti fedha za kukaa kwenye vikao zifutwe, wakati wamepokea fedha hizo miaka mitano iliyopita huko nyuma.
…Sasa kama kweli wanasimamia wanachokisema warejeshe fedha hizo, hawa ni waapinzani tu na wataendelea kuwa wapinzani milele,” alisema Sitta.
Wabunge waimba CCJ
Wakati Sitta akizungumza zilikuwa zikisikika sauti zikichombeza kwa chini kwa kuimba CCJ, CCJ, CCJ baada ya Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kumaliza kuzungumza, Mwenyekiti wa Bunge alilazimika kusitisha majaridiano hadi jioni.
Awali, Kafulila katika mchango wake alisema Serikali imejenga nyufa kati ya tabaka la masikini na viongozi wa umma, na kwamba hiyo ndiyo sababu inayofanya itoe uzito mdogo kwa sekta ya afya kwasababu wao wanatibiwa nje.
“Kutokana na nyufa mliyotengeneza siyo rahisi kwa mtoto wa, Sitta kutibiwa hospitali moja na mtoto wa Kalumanzira kule Kigoma,” alisema.
Kafulila akataa taarifa za Mawaziri
Baada ya kusema hivyo,Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige alitoa taarifa kwamba watoto na familia yake wanatibiwa kijijini kwake.
Lakini Kafulila aliikataa taarifa hiyo. Baada ya kusema hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu akatoa taarifa kuwa siyo kweli kwamba viongozi wanatibiwa hospitali tofauti na wanazotibiwa tabaka masikini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti namheshimu na nampenda sana mheshimiwa mbunge kama mtoto wangu, lakini asitoe kauli kwa ujumla. Hivi karibuni Baba yangu mimi alikuwa mgonjwa na akatibiwa na kulazwa kwenye hospitali ya Wilaya kule Hanang’.
…Mimi mwenyewe na familia yangu tunatibiwa kwenye hospitali za serikali, hivyo Mbunge asitoe kauli kama hiyo,” alisema Dk. Nagu.
Mwenyekiti wa Bunge, Mhagama alipomtaka, Kafulila kukubali taarifa hiyo au kuikataa, lakini mbunge huyo aliikataa na kueleza kuwa “nilichosema ni sahihi, mbunge na familia yake anatibiwa ndani ama nje bure, ndiyo maana hatuboreshi sekta ya afya, huo ndiyo ukweli wenyewe,” alisema Kafulila.
Katika michango yake mingine, Kafulila aliitaka serikali kuelewa kuwa inawatumikia binadamu ambao wanastahili kuishi, hivyo iboreshe sekta ya afya ili kuwawezesha wananchi kuipata pindi wanapokuwa wagonjwa.
Mbunge huyo alimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda wakati mwingine anapokwenda kwenye Baraza la Mawaziri kukataa anapotengewa bajeti ndogo.
“Mheshimiwa Waziri hii bajeti ni ndogo sana, unapoenda kwenye ‘cabinet’ fedha hizi zikatae hatuwezi kujadili asilimia 2.2 tu, ikiwezekana kuwa tayari kujiuluzu na si kukubali kiasi hiki kidogo, hapa hata tukikuchania shati bado fedha hazitoshi,” alisema.
Pia alisema serikali iboreshe vyanzo vyake vya mapato ili kuacha tabia ya kutegemea fedha za nje na badala yake fedha nyingi ziwe zinatengwa za ndani kwani wakati mwingine fedha za wahisani zinachelewa kuja jambo ambalo linasababisha wananchi kukosa kupata huduma ya afya.
“Hatuwezi kutegemea fedha za nje, sisi tumejiegemeza kwenye wafadhili ambao wanatupangia masharti kwamba fedha wanazotoa ziende kwenye Ukimwi, wakati ukweli ni kwamba kuna magonjwa mengine yanayoua zaidi.
…Tumejiegemeza kwenye ufadhiri, sisi asilimia 97 tunategemea ufadhiri, tuache kununua mashangingi kwa ajili ya wakurugenzi tuwekeze kwenye afya, sisi ni taifa la saba kwa misaada duniani hii ni aibu,” alisema.
Bajeti hiyo ambayo ilizua taflani hiyo ilitarajiwa kuhitimishwa jana jioni ambapo bunge litakaa kama kamati kupitisha kifungu baada ya kifungu.