Na Tumainiel Seria
KADI za Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana ziligombewa na wananchi wa Wilaya ya Same wanaohudhuria mikutano ya chama hicho kwa ajili ya kukiimarisha chama.
CHADEMA inafanya mikutano ya kukihimarisha chama inayoendeshwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), John Heche na viongozi wengine wa chama hicho wakiwemo makada maarufu waliohamia CHADEMA wakitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, mkoani Arusha, James Ole Millya na Mjumbe wa NEC ya CCM kutoka Arusha, Ally Bananga ni miongoni mwa makada wanaounguruma katika mikutano hiyo ya kukihimarisha chama cha CHADEM, wilayani Same.
Mkutano wa jana ulishuhudia idadi kubwa ya wakazi waliohudhuria mkutano huo wakigombea kadi zilitolewa kama ofa na Millya aliyetoa kadi 10 kwa vijana huku aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akitoa ofa ya kadi 10 kwa akina mama.
Miongoni waliohamia katika chama hicho kwenye mkutano huo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TLP Same, Heriel Msolo ambaye alirudisha kadi ya TLP na kupewa kadi ya CHADEMA na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche.
CHADEMA wanaziara ya kichama Wilayani Same kwa siku nne, kuanzia jana na wanatarajia kumaliza Jumatatu chini ya Mwenyekiti wa John Heche. Mikutano hiyo inafanyika maeneo tofauti ya Wilaya ya Same ikiwa na lengo la kukihimarisha chama. Mkutano wa jana ulifanyikia viwanja vya Kwasakwasa Mjini Same majira ya saa 9 hadi saa 12 jioni.
Katika mkutano huo, Lema aliwataka watanzania kutokubali kugwanywa na wanasiasa kwa misingi ya udini na ukabila au ukanda na kueleza kwamba CHADEMA haipiganii maslahi ya kundi lolote katika hayo. Alisema hata yeye hapiganii maslahi yake binafsi bali ya Watanzania.
Heche aliwataka Watanzania kujitokeza kutoa maoni yao kwa Tume ya Katiba na kuelekeza kuwa wapinge nafasi za Ukuu wa mikoa na wilaya kuteuliwa na mtu mmoja yaani Rais wa Tanzania. Ameeleza kuwa madaraka ya rais ni makubwa na mambo mengi yameachwa kwa mtu mmoja, hali inayohitaji marekebisho ili kuwe na uwajibikaji wa pamoja.
http://arusha255.blogspot.com