Na Mwandishi Wetu
JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ) limetoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 25, kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40.
Akikabidhi msaada huo jijini Dar es Salaam Brigedia Jenerali Cylil Ivor Mhaiki kwa Niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, amesema vyakula hivyo ni kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko hayo.
Amesema JWTZ linatambua matatizo ambayo yana wakabili wananchi ambao wamekumbwa na mafuriko hayo pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka pamoja na mwaka unaotarajia kuanza siku chache zijazo
Amesema msaada huo ni Mchele kilo 75,000 sawa na gunia 75, Maharage kilo 1600 sawa na maguni 16, Sukari kilo 1600 sawa na gunia 16 na Majani ya chai kilogram 224.
Mkuu huyo wa mkoa amemwambia Brigedia Cylil Ivor Mhaiki kuwa Serikali tayari imeshafanya tathimini ya kuwagawia viwanja wale wote ambao wamekumbwa na maafa hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amepokea misaada hiyo na kuwashukuru wote waliojitolea kuwasaidi waathirika wa mafuriko na kutoa wito kwa taasisi nyingine kujitokeza kuwasaidia waadhirika hao.