RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete, amelisifia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutaja mafanikio yake makuu katika miaka 50 ya uhai wake, akisisitiza kuwa ni Jeshi imara na bora linaongozwa na misingi ya uzalendo, utii na nidhamu ya hali ya juu.
Rais pia amesema kuwa kwa amani, utulivu na usalama ambao umekuwepo katika Tanzania kwa miaka 50 iliyopita umechangiwa sana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. JWTZ lilizaliwa Septemba Mosi, 1964. Akizungumza na maelfu ya wapiganaji na wananchi kwenye Sherehe za Miaka 50 ya Jeshi hilo kwenye eneo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete alisema kuwa uzalendo na nidhamu ni mambo ambayo yanalitofautisha JWTZ na majeshi mengine mengi duniani mambo yaliyoyashinda majeshi ya nchi nyingi hususan katika Afrika.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza baada ya kushuhudia Zoezi la Medani la Operesheni Maliza Matata ambalo limeshirikisha mamia ya wapiganaji na maofisa ambako zimetumika silaha za moto kwa njia ya ndege za kivita, vifaru, makombora na risasi. Zoezi hilo limeshirikisha maofisa na askari kutoka Makao Mkuu ya Jeshi, Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Maji, Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Akiba.
Rais Kikwete amewaambia wapiganaji nao na maofisa wao ambao walikuwa ni pamoja na wakuu waliopita wa Jeshi hilo kuwa moja ya mafanikio makubwa ya Jeshi hilo ni kusimamia na kutekeleza majukumu yake iwe ni wakati wa amani ama wakati wa vita, tena kwa weledi mkubwa. Rais Kikwete ameyataja mafanikio machache ya Jeshi hilo kuwa ni pamoja na kushiriki na kufanikisha harakati za Ukombozi Barani Afrika kwa kufundisha majeshi ya Vyama vya Ukombozi, na kushiriki moja kwa moja kwenye vita vya Ukombozi mwa Kusini mwa Bara la Afrika katika Mozambique, Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini.
Rais pia amesema kuwa JWTZ limelinda uhuru na mipaka ya nchi kwa vitendo kwa kuyapiga majeshi ya uvamizi ya Idd Amin na kuweka historia kwa kuwa Jeshi lililopigana na jeshi la nchi nyingine na kuliangamiza kabisa. Kikwete pia amesema kuwa JWTZ limeshiriki kikamilifu kwenye operesheni za kulinda amani katika nchi za Liberia, Darfur (Sudan), Lebanon, Ivory Coast, Visiwa vya Shelisheli, Visiwa vya Comoro na hivi karibuni kuyapiga na kuyatoa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) majeshi ya waasi wa M23.
Rais pia amesema kuwa JWTZ limeshiriki kikamilifu shughuli za uokoaji na hususan katika majanga ya ajali kama za Meli za MV Bukoba na kule Zanzibar na kwenye majanga ya mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini. Rais amesema kuwa mamilioni ya Watanzania wamenufaishwa na huduma za elimu na afya ambazo Jeshi hilo linazitoa kupitia shule na hospitali zinazomilikiwa na Jeshi na pia limeshiriki katika kukuza elimu ya kujitegemea kwa vijana kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Rais Kikwete amesema kuwa katika miaka yote 50, JWTZ halijawahi kuacha malengo yake makuu ya kuanzishwa kwake.
“Limebakia la ulinzi wa wanchi siyo uvamizi. Limebakia Jeshi linalotokana na Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya Wananchi wa Tanzania. Limebakia Jeshi la Ukombozi na kulinda amani lililotumika kwenye harakati za Ukombozi wa Afrika na kulinda amani duniani.”