JUMLA ya watoto 13,266 wenye umri chini ya miaka 10 wamenufaika mkoani hapa
na huduma za afya zitolewazo na taasisi ya Kikorea ijulikanayo kama
UHIC (United Help for International Children) .
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo kanda ya Tanzania, Lee Kwiwoon alitoa taarifa
hiyo hapa mwishoni mwa juma lililopita katika mkutano uliojumuisha
madaktari, manesi na wahudumu wa afya kutoka wilaya tatu za mkoa huu,
ambazo zimelengwa katika mradi wa taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema lengo la kuanzisha taasisi hiyo ni kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo mbalimbali ya kiafya yanayowapata wenye umri chini ya
miaka 10.
Aliwaeleza wanasemina hao kwamba watoto wengi walio katika umri chini ya miaka 10 hukumbwa na magonjwa mengi, hasa malaria, upungufu wa damu na utapiamlo.
Magonjwa mengine ni pamoja na kifua, kuzaliwa njiti na
kuharisha.
Lee aliwaambia maofisa na manesi pamoja na wahudumu wa afya kwamba jukumu
kubwa la taasisi yake ni kuzuia magonjwa yanayowanyemelea zaidi watoto
wadogo pamoja na kuhakikisha watoto hao wanakua katika afya
bora.
Alifahamisha kwamba taasisi hiyo ya UHIC imeanzisha mradi ujulikanao Keepers’ ambao unawafundisha na kuwapatia mafunzo vijana wanaotoa huduma ya kuokoa
maisha ya watoto kutoka janga la njaa, maradhi na kuwasaidia waishi
katika mazingira mazuri ya kiafya.
“Afya na uzuiaji wa magonjwa yawapatayo watoto wengi mkoani Tanga ni suala
linalozungumzika na hivyo kuwafanya wadau kuamua kujitolea kuanzisha
taasisi zitakazosaidia kuondoa adha hiyo kwa watoto wetu”, alisema
Lee.
Mkurugenzi huyo alibanisha kuwa taasisi ya UHIC ni ya kimataifa iliyoanzishwa kwa
lengo la kutoa huduma endelevu za afya kwa watoto waishio maeneo ya
vijijini (pembezoni) mkoani hapa.
Alisema wamechagua wilaya tatu ambazo ni Pangani, Muheza na Tanga kuwa za mfano katika kuanza na mradi huo ambapo jumla ya vijiji 27 vitahusika.
Alisema taasisi yake ina jukumu la kugawa dawa na kwamba wahudumu 24
tayari wamekwishapatiwa mafunzo ya kuhudumia watoto hao katika vijiji
husika.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Maggid alisema mkoa umepoteza maisha ya watoto wapatao 653 kutokana na magonjwa mbalimbali, yakiwemo malaria, kikohozi, upungufu wa damu na
kuharisha.
Pamoja na kupongeza msaada huo wa Korea akisema kuwa umefika wakati
ukihitajika sana, lakini akataka wataalamu wanaopelekwa kwenye vijiji
hivyo wapewe ushirikiano unaofaa.
Mapema, akifungua semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa waTanga, Mayassa Hashim
alisikitishwa na vifo hivyo ambapo alisema vingeweza kuzuilika kwa kutoa
elimu ya kutosha kwa wazazi .
Hata hivyo, Mayassa ambaye pia ni OfisaElimu wa Mkoa, alieleza matumaini kwamba ujio wa taasisi hiyo pamoja na madawa na wataalamu wao itasaidia kuondoa vifo visivyotarajiwa vya watoto wadogo.
Picha na stori kwa hisani ya Tanga Raha Blog