Jukwaa la Wahariri Tanzania Lakutana, Lalaani Kufungiwa Magazeti

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda

Kikao cha Wajumbe wa Jukwaa la Wahariri kilichofanyika leo, Alhamisi, Oktoba 3, mwaka 2013, kimejadili uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Wajumbe wa kikao hicho wamesikitishwa kwa hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya magazeti hayo. Baada ya mjadala wa kina, wajumbe wa Jukwaa wameazimia yafuatayo.

1. Kupinga uamuzi wa serikali:

Jukwaa linapinga hatua hiyo dhidi ya magazeti hayo kwa sababu adhabu hiyo imetolewa kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau kwa miaka mingi sasa.

Hii ni moja ya sheria ambazo Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza ifutwe kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukiuka misingi ya haki za binadamu, utawala bora na kwenda kinyume cha Katiba ya nchi pamoja na maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu.

Hivyo, tunaungana na taasisi nyingine kupinga adhabu hii kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania na wakati huo huo tukikumbushia kifungo cha gazeti la Mwanahalisi kwa sababu sheria iliyotumika haifai.

2. Tunalaani kufungiwa kwa magazeti hayo:

Utaratibu uliotumiwa na serikali kwa kujigeuza kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na mtoa adhabu kamwe haukubaliki katika jamii yoyote iliyostaarabika kwa sababu ni kinyume cha utaratibu wa kutoa haki ya asili (natural justice). Hili si jambo la kuendelea kufumbiwa macho na jamii ambayo inafuata misingi ya Kidemokrasia na utawala bora.

Hivyo, tunalaani kwa nguvu hatua hizi zilizochukuliwa kwa kukiuka misingi hii yote, hasa ukizingatia kuwa ni serikali hii ambayo imesaini makubaliano ya kimataifa kuhusu uwazi katika uendeshaji wa serikali (open government initiative).

Nini kifanyike:

Tunafahamu kuwa kuna kesi ya kuipinga sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo ilifunguliwa mwaka 2009. Ni jambo la bahati mbaya na kusikitisha sana kuwa hadi hivi sasa, miaka minne baadaye, bado kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kwa sababu haijapangiwa majaji.

Jukwaa la Wahariri linapenda kutoa mwito kwa Mhimili wa Mahakama kurekebisha kasoro hii kwa kupanga majaji kwa ajili ya kuisikiliza. Kufanya hivi kutahakikisha si tu haki kutendeka, bali pia haki kuonekana inatendeka. Kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki.

Tunasikitika zaidi kwamba serikali inaendelea kutumia sheria hii kandamizi huku ikiwa imeikalia kwa miaka mingi sasa miswada ya sheria mbili muhimu zinazohusu haki za habari bila ya kuziwasilisha bungeni. Kwa hiyo tunaitaka serikali kuwasilisha miswada hiyo bungeni ili kupatikana kwa sheria mpya ya kusimamia tasnia ya habari nchini.

Hitimisho:

Hivyo basi, tunatoa mwito kwa serikali kuyafungulia magazeti hayo.