JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limeitaka Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli kufufua mchakato wa Katiba Mpya ambao limedai ulitelekezwa kimya kimya bila maelezo ya kueleweka. Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam katika ofisi zao ameitaka Serikali kufufua mchakato huo na kuanzia na kuitisha mkutano mkuu maalumu wa kitaifa ili ujadili suala hilo kabla ya kuendelezwa.
Aliiomba Serikali kwa kuanzia itangaze kwenye gazeti la Serikali mara moja kuendelea na mchakato huo, ambao haukusitiswa bali uliachwa ujisitishe wenyewe bila maelezo yoyote ya kueleweka. Kibamba amemuomba Rais Magufuli kubeba ujasiri na kurejesha mchakato wa Katiba Mpya uliotelekezwa.
Alisema kwa muonekano uliopo kwa sasa Serikali wala Wizara husika inaonekana haina mpango wowote wa kulishughulikia suala la Katiba Mpya hadi muda huu, huku muda ukizidi kusonga. Alisema Serikali ya sasa chini ya Dk Magufuli inajitahidi kufanya vizuri kiusimamizi wa masuala ya fedha ni vema ikajenga mifumo ya kudumu kwa kuja na katiba mpya kuliko kungojea busara za kiongozi awaye madarakani. Alisema dalili hizo zinajidhihirisha kwa kile kutopanga wala kutenga bajeti yoyote kwa ajili ya kufufua mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema JUKATA itaendelea kupaza sauti kwa kila hali hadi kuhakikisha mchakato huo unaendelea ili taifa lipate misingi ya kudumu na stahiki ya kuliongoza kwa matakwa ya wananchi wenyewe na si busara za kiongozi aliepo madarakani muda huo. Alisema kwa sasa wamebaini kuna mtindo wa kuminya uhuru wa kujieleza kwa kutoa vitisho jambo ambalo aliashirii utawala bora.