JOTO la siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka huu limeanza kupanda wilayani Rombo baada ya mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Fraterni Michael Lasway kutangaza nia ya kugombea Jimbo la Rombo kupitia tiketi ya chama hicho.
Lasway ambaye kwa sasa ni Ofisa Manunuzi kutoka Hospitali ya Aga Khani ya jijini Dar es Salaam ametangaza uamuzi huo wakati alipozungumza na mtandao huu ambapo alisema kuwa anataka kuungana na wananchi wa Rombo kuwaletea maendeleo.
Alisema kuwa sababu hasa iliyomsukuma kuwania nafasi hiyo katika Jimbo la Rombo ni kutaka kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya hiyo, ambapo alifafanua kuwa licha ya Wilaya ya Rombo kuwa na rasilimali nyingi lakini bado wananchi wake ni masikini.
“Dhamira yangu kuu hasa najiuliza kwanini wananchi wa Rombo si matajiri wakati wanazo rasilimali zinazoweza kuwafanya kuwa matajiri, ukiangali Wilaya ya Rombo ina rasilimali nyingi kuliko wilaya nyingine…naamini imekosa siasa safi na uongozi bora ili kuweza kusimamia rasilimali hizo na wananchi kupata maendeleo…ndipo nikaona mimi naweza kusimamia hilo,” alisema Lasway.
Lasway alivitaja vipaumbele vyake atakavyovisimamia ni suala la elimu, kilimo, afya pamoja na kuhakikisha uchumi wa wananchi unaimarika kwa ujumla ili kuwanufaisha Watanzania.
“…Muda utakapofika nitawaeleza wanachi vipaumbele vingi zaidi, lakini lazima kujipanga kuboresha elimu maana bila elimu watu hawawezi kufanya shuguli zao kwa umakini. Vivyo hivyo bila afya njema wananchi hawawezi kushiriki kwenye kilimo na mambo mengine ya maendeleo vema,” alisema.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kujitkeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pindi muda utakapofika na pia wajitokeze kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Jimbo la Rombo kwa sasa linaongozwa na Mbunge, Joseph Selasini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).