MSANII Lucas Mhavile a.k.a Joti baada ya kukaa kimya kwa muda sasa ameibuka na filamu yake mpya inayojulikana kama Joti Sanduku la Babu ambayo amecheza katika uhusika tofauti katika filamu hiyo.
Akizungumzia filamu hiyo Joti alisema kuwa ametoka kivingine kabisa katika filamu hiyo, na kujinasiku kuwa kitu alichofanya kwenye filamu hiyo haijawai kutokea wala kufanywa na mtu yoyote yule katika tasinia hii ya filamu nchini.
Joti amewataka wapenzi wa filamu nchini kukaa mkao wa kula kuipokea filamu hiyo ambayo itakuwa ikisambazwa na kampuni ya Proin Promotions ya jijini Dar es Salaam. “…Wapenzi wangu wakae mkao wa kula tu kwani wakati wowote kuanzia sasa itakuwa inaingia sokoni, filamu hii si yakukosa maana unambiwa uzee mwisho Chalinze mjini kila mtu honey…,” alisema.
Aidha aliwaomba wapenzi wa filamu kuhakikisha wananunua nakala halisi ya filamu hiyo pindi itakapotoka na kuachana na wale wote wasiowatakia mema wasanii kwa kuendekeza filamu za zisizo halisi jambo ambalo linaua tasnia ya filamu.
Aliongeza kuwa filamu hiyo imebeba mambo matatu muhimu; ambapo la kwanza ni inaburudisha, ina elimisha na kutoa ujumbe muhimu kwa jamii inayotuzunguka. Filamu hii ni ya kwanza tangu Joti aweke kando mambo ya filamu na kujiingiza katika mambo ya uchekeshaji kupitia luninga.