Na Mwandishi Maalumu, Lindi
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kazi kubwa ya viongozi ni kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa matatizo na kero za wananchi, na si vinginevyo, kwani uongozi ni utumishi wa wananchi.
Amesema kila kiongozi kwa ngazi yake ana wajibu wa kukabiliana na kumaliza matatizo na kero za wananchi walio chini yake, badala ya kusubiri uongozi wa juu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi wake.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo Agosti 20, 2011 jioni alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Lindi baada ya kula nao futari mjini Lindi na hivyo kutumia nafasi hiyo kujua namna tatizo la maji mkoa huo linavyopatiwa ufumbuzi.
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Lindi alitoa kauli hizo baada ya kukutana na viongozi wa Mkoa wa Lindi kutaka kujua hali ya upatikanaji maji katika mji wa Lindi na jitihada za uongozi wa Mkoa huo kukabiliana na tatizo hilo.
Rais Kikwete ameelezea umuhimu wa viongozi kutimiza wajibu wao baada ya kuwa amejulishwa kuwa moja ya sababu ya kukosekana maji ya kutosha katika Mji wa Lindi ni kukosekana kwa kiasi cha sh. 25,000,000 kwa ajili ya kununulia mafuta ya dezeli kusukuma mitambo ya umeme kwenye chanzo cha umeme cha Kijiji cha Kitunda.
Rais Kikwete alihoji inakuwaje uongozi mzima wa Mkoa wa Lindi ukiwamo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Maji la Mji wa Lindi (LUWASA), Halmashauri ya Mji wa Lindi na ule wa Mkoa wanashindwa kutafuta kiasi cha sh. 25,000,000 ili kuwapatia wananchi maji.
Rais Kikwete katika kuhakikisha kuwa fedha hizo haziendelei kuwa kikwazo cha upatikanaji wa maji, aliagiza ngazi mbalimbali za Mkoa wa Lindi kukutana leo, Jumatatu, Agosti 22, 2011, kuhakikisha kuwa dizeli inapatikana kuwezesha mitambo ya Kitunda kufanya kazi.
Ili kufuatilia kujua hali halisi ya upatikanaji maji, Agosti 21, 2011, alitembelea chanzo cha maji cha Mji wa Lindi kilichopo katika Kijiji cha Kitunda, Kata ya Msinjahili, Halmashauri ya Lindi ambako alielezwa hali ya upatikanaji maji kutoka katika chanzo hicho na kujionea hali halisi ya mitambo.
Kwenye chanzo hicho cha maji cha Kitunda, Rais Kikwete ameonyeshwa mashine mbili za kusukumia maji, akakagua visima viwili vikubwa ambako yanavutwa maji na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
Rais Kikwete ameelezwa kuwa hali ya upatikanaji maji katika Mji wa Lindi siyo nzuri kwa sababu hadi Julai mwaka huu ni kiasi cha lita 550,000 tu za maji zilizokuwa zinawafikia wakazi 92,000 wa Mji wa Lindi kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 11 tu ya mahitaji ya maji ya mji huo. Rais Kikwete ameelezwa kuwa Mji wa Lindi unahitaji kiasi cha lita 3,000,000 za maji kwa siku.
Wakati akizungumza na wananchi wa Kitunda, Rais Kikwete amewaelekeza viongozi wa Mkoa wa Lindi kuhakikisha kuwa wananchi wa kijiji hicho cha Kitunda pia wanapata maji kutokana na chanzo hicho cha maji.
Rais ametoa agizo hilo baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa pamoja na kwamba maji yanatoka kwenye kijiji hicho, bado wananchi wa kijiji hicho hawapati maji kutokana na chanzo hicho.