JK: Salama ya Burundi ni Kuheshimu Katiba na Sheria

Rais Dk.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea Maua kutoka kwa watoto waliokuja kumlaki katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura ambapo alianza ziara ya kikazi ya siku mbili.

Rais Dk.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea Maua kutoka kwa watoto waliokuja kumlaki katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura ambapo alianza ziara ya kikazi ya siku mbili.


Rais Kikwete akiwa na Mwenyeji wake Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi jijini Bujumbura. Picha zote na Ikulu.

Rais Kikwete akiwa na Mwenyeji wake Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi jijini Bujumbura. Picha zote na Ikulu.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amewashauri viongozi na wananchi wa Burundi kufanya mambo manne muhimu ili kutuliza hali ya sasa ya kisiasa katika nchi hiyo na hivyo kuepusha ukosefu wa utulivu wa kisiasa na hata kuzuka kwa machafuko.

Rais Kikwete amesema kuwa mambo hayo manne ni pamoja na kwa wananchi na viongozi wa Burundi kuheshimu, kwa vitendo na imani, Katiba ya nchi hiyo, kuheshimu Makubaliano ya Arusha yaliyozaa amani katika Burundi na pia kuheshimu Sheria za Uchaguzi za nchi hiyo.

Rais Kikwete pia amewataka viongozi na wananchi wa Burundi kujiepusha na kuvutiwa na matumizi ya nguvu katika kutafuta majawabu ya matatizo yao, jambo ambalo linaweza kuiingiza nchi hiyo katika matatizo makubwa zaidi.

Jambo la tatu ambalo Rais Kikwete amewashauri viongozi na wananchi wa Burundi ni kutumia mazungumza na majadiliano, kwa kadri inavyowezekana, akisisitiza kuwa hakuna ukosefu wa watu wenye busara na taasisi ambazo zinaweza kusaidia kusimamia na kuendesha mazungumzo na majadiliano hayo.

Rais Kikwete amesema kuwa jambo la nne ambalo viongozi na wananchi wa Burundi wanastahili kufanya katika hali ya sasa ni kutumia Sheria za Burundi inapotokea kuwa baadhi ya wananchi wakahisi kuwa Sheria za Uchaguzi za Burundi zinakiukwa.

Rais Kikwete ametoa ushauri huo, Machi 19, 2015, wakati alipohutubia Bunge la Afrika Mashariki katika Ukumbi wa Bunge la Burundi katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Bujumbura. Hotuba ya Rais Kikwete ambayo hutolewa kila mwaka na Mwenyekiti wa Jumuiya ilihusu hali ya sasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki – The State of the East African Community Address.

Rais Kikwete amewaambia Wabunge hao wa Bunge la Afrika Mashariki na mamia ya wageni waalikwa: “Kwa kaka zangu na dada zangu wa Burundi, pengine niseme kuwa ninatambua wasiwasi kuhusu mchakato wa uchaguzi ambao uko mbele yenu. Kuna minong’ono na hofu kwamba amani na utulivu ambao umekuwepo katika Burundi kwa miaka karibu 15 sasa huenda ikapotea. Wengine wanasema yanaweza hata kuwepo machafuko. Tunaomba Mungu haya yasitokee.”

Amesema Rais Kikwete: “Hivyo, nawaomba  viongozi wa Burundi – viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini, viongozi wa kijamii pamoja na taasisi za kijamii kufikiria kufanya yale ambao nashauri, yanaweza kusaidia nchi yetu hii nzuri, kubakia na utulivu na amani.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Tuna imani nanyi kwamba mnao uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na kuzipatia majawabu. Huko nyuma mmepata kukabiliana na changamoto kubwa zaidi na mkazimaliza. Sioni kwa nini mshindwe zamu hii. Jipeni ujasiri, jipeni utashi wa kisiasa, na yote yatakuwa sawa.”

“Nataka kuwahakikisheni kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iko tayari kusaidia katika hili. Tutakweda sambamba nanyi kwa kila hatua, njia nzima, kama ambavyo tumepata kufanya huko nyuma.”

Hali ya wasiwasi ya sasa ya kisiasa katika Burundi inatokana na tofauti za tafsiri ya Katiba, Sheria za Uchaguzi na Makubaliano ya Arusha kuhusu kama Rais Pierre Nkurunziza anayo haki ya kusimama kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu baada ya kuwa Rais wa Burundi kwa miaka 10 sasa.