RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali yake inazikumbuka ahadi zote zilizotolewa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita na imejiwekea utaratibu wa kuzitekeleza.
Rais Kikwete ameyasema hayo Julai 25, 2011 katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara katika mkutano wa hadhara ambako ameanza ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa Rais wa Tanzania na kukichagua Chama Cha Mapinduzi kuongoza nchi yetu.
“Nashukuru kwa kunichagua, tuliomba utumishi tutawatumikia, kila tulichoahidi tunakumbuka na tumeweka utaratibu wake wa kuzitekeleza ahadi zote”. Rais amesema.
Rais amezitaja baadhi ya ahadi za mkoani Mtwara kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mtwara/Tandahimba hadi Masasi kwa kiwango cha lami, kumaliza tatizo la maji mkoani Mtwara, hospitali na ukarabati wa bandari ya Mtwara, uchimbaji wa gesi na ujenzi wa kiwanda cha mbolea.
Rais amesema “katika ahadi zote utekelezaji umeanza na katika bajeti ya mwaka huu tayari pesa zimetengwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu”, amesema na kuongeza kuwa hata utatuzi wa shida ya maji tayari utekelezaji uko katika hatua za mwanzo ambapo vijiji vinavyozunguka mji wa Mtwara vitapata maji kwanza.
Ahadi zingine katika mkoa wa Mtwara ni pamoja na kutatua tatizo la walimu ambapo tayari shilingi bilioni 35.2 zimetengwa kwa ajili ya kujenga shule za walimu Tanzania nzima.
Rais pia ametembelea bandari ya Mtwara ambapo ameongea na viongozi wa bandari, wadau wa kubwa wa bandari hiyo na wawekezaji wanaowekeza katika shughuli za gesi mkoani humo.
Rais Pia amezindua Shule ya Sekondari ya Mustafa Sabodo na kuzungumza na wanafunzi ambapo amewashukuru wananchi kwa kuichagua CCM na kuwaeleza kuwa haitawaangusha katika kuleta maendeleo ya Mkoa wa Mtwara.
Rais pia amemshukuru Mustafa Sabodo kwa msaada wake wa kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana na kuwahimiza kusoma. Rais anaendelea na ziara Mtwara Vijijini na baadaye Wilaya ya Tandahimba.