JK-Nilazima tutafute Shuruhisho la kudumu Congo(DRC)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho
Kikwete amependekeza Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze kutafuta suluhu
mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa njia ya
mazungumzo badala ya kutegemea ufumbuzi kwa njia ya kijeshi pekee.
Rais Kikwete ametoa pendekezo hilo , Jumapili, Mei 26, 2013, wakati
wa mkutano wa kwanza wa Mchakato wa Kikanda wa Usimamizi wa Amani,
Usalama na Ushirikiano katika DRC na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGRL)
uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), wakuu wa nchi
wanachama wa ICGRL, na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) na limekubaliwa.
Mkutano huo umefanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia ambako Rais Kikwete na viongozi wengine
wanaohudhuria Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU ambao
umefunguliwa asubuhi ya leo.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo
zuri na la maana sana kuwa na Jeshi la Kulinda Amani katika DRC –
Force Intervention Brigade – katika Congo chini ya Umoja wa Mataifa
ambako nchi za SADC ikiwamo Tanzania inachangia majeshi lakini kuwepo
kwa jeshi hili mashariki mwa Congo hakutatosha kuleta suluhu ya kudumu
nchini humo.
“Jambo hili tulilofanya ni zuri sana. Tunaendelea na maandalizi ya
kupeleka jeshi mashariki mwa DRC chini ya UN kama ilivyokubaliwa.
Tunaamini kuwa katika muda mfupi, jeshi hili litakuwa la msaada
kijeshi, lakini haliwezi kuwa suluhu ya kudumu kwa tatizo la DRC –
majibu ya tatizo hili lazima yawe ya kisiasa,” amesema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Nia iwe ni kusikiliza pande zote, kusikiliza malalamiko yote ya
kisiasa kama yapo, malalamiko ambayo ndiyo yanazaa mapambano ya silaha
katika nchi hii jirani. Nia ni kujenga mazingira ya kuelewana na hivyo
kuwezesha mazungumzo kuwa njia muhimu zaidi ya kutafuta mwafaka.”
Kufuatia maelezo yake, Rais Kikwete amependekeza kuwa katika hatua ya
kwanza Jumuiya ya Kimataifa iunge mkono kwa njia zote mazungumzo
yanayoendelea sasa kati ya Serikali ya DRC na waasi wa M23 mjini
Kampala, Uganda ili yaweze kufanikiwa na kuleta maridhiano kati ya
pande hizo mbili.
“Haya ni mazungumzo muhimu sana. Yalitakiwa kuwa ya wiki tatu na sasa yamefikia mwezi wa sita ni muhimu yaendelea na sote katika Jumuiya ya
Kimataifa tuyaunge mkono kwa sababu tukifanikiwa kupata maelewano
kutokana na mazungumzo hayo tutakuwa tumepiga hatua kubwa.”
Rais Kikwete amesema kuwa aina ya pili ya mazungumzo yanatakiwa ni
kujenga mazingira ambako vikundi vya waasi ambavyo vimejificha katika
DRC na vinaendesha uasi dhidi ya nchi zao za asili – ADF (Uganda) na
FDRL (Rwanda) vinashiriki katika mazungumzo na nchi zao za asili ili
kujenga maelewano.
Aina ya tatu ya mazungumzo, kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni yale kati
ya Serikali ya DRC na vikundi vingine vya ndani vya waasi kama vile
Mai Mai na vingine. “Hivi viko vingi na vina malalamiko yao na ni
muhimu nayo yasikilizwe na yatafutiwe ufumbuzi wake.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na
viongozi wawili wa Afrika – Rais Hifikapunye Pohamba wa Namibia na
Rais Mohamed Morsy wa Misri.
Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete na Rais Pohamba wamezungumzia masuala yanayohusu SADC wakati mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Morsy wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Misri.