Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni kweli nchi za Afrika bado zinahitaji misaada ya maendeleo lakini wajibu wa kuendeleza nchi hizo unabakia mikononi mwa nchi hizo na siyo kwa mtu mwingine yoyote wakiwamo wafadhili.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wakati umefika kwa Tanzania na Afrika Kusini kutumia uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizo ili kujenga mahusiano imara na ya karibu zaidi ya kiuchumi kati ya nchi hizo.
Pia, Rais Kikwete kwa mara nyingine amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kujitokeza kwa wingi zaidi kuanzisha vitega uchumi na kuwekeza katika uchumi wa Tanzania kwa sababu ya vivutio vikubwa vya kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Hayo yameelezwa na Rais Kikwete leo, Jumanne, Julai 19, 2011 kwenye siku ya kwanza ya ziara ya kihistoria ya siku tatu ya Rais Kikwete katika Afrika Kusini, ziara ya kwanza ya kidola kufanywa na Rais wa Tanzania katika historia ya Afrika Kusini ya kidemokrasia tokea mwaka 1994.
Katika siku yenye shughuli nyingi, Rais Kikwete ameanza siku ya leo kwa kupokelewa rasmi kwenye Majumba ya Muungano (Union Buildings) mjini Pretoria, ambako ndiko Makao Makuu ya Serikali ya Afrika Kusini.
Rais Kikwete akifuata na Mama Salma Kikwete wamewasili kwenye Majumba hayo kiasi cha saa mbili na dakika 20 asubuhi ambako amepokelewa na mwenyeji wake, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na mkewe. Sherehe hizo za mapokezi zilizochukua kiasi cha nusu saa zilipambwa na gwaride rasmi la Jeshi la Afrika Kusini na mizinga 21 ya heshima kwa kiongozi huyo wa Tanzania.
Sherehe za makaribisho zilifuatiwa na mazungumzo ya faragha kati ya viongozi hao wawili, mazungumzo ambayo yamefuatiwa na mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Baadhi ya Mawaziri wa Tanzania walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhe. Profesa Jumanne Maghembe, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Cyril Chami.
Wengine ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Fedha, Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini, Balozi Radhia Msuya. Serikali ya Afrika Kusini imewakilishwa na Mawaziri Tisa, Naibu Mawaziri wawili na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Balozi Chiliza.
Kwenye mazungumzo hayo, Rais Zuma ameishukuru tena Tanzania kwa msaada mkubwa ambao nchi hiyo ilitoa kwa wapigania Uhuru wa Chama Tawala cha ANC na vyama vingine vya kupigania uhuru Kusini mwa Afrika.
Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kuwaelezea viongozi hao waandamizi wa Serikali ya Afrika Kusini kuhusu nafasi za uwekezaji ambazo zinapatikana katika Tanzania na akawaomba viongozi hao wa Afrika Kusini kusaidia kuwashawishi wawekezaji wa nchi hiyo kukubali kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Hadi sasa kiasi cha makapuni 178 ya Afrika Kusini yamewekeza katika uchumi wa Tanzania kwa thamani ya kiasi cha dola za Marekani milioni 592.82. Miradi hiyo imetengeneza kiasi cha ajira 18,438 kwa ajili ya Watanzania.
Rais Kikwete amesema kuwa baada ya mahusiano ya kihistoria na ya miaka mingi ambayo yalijengwa kwa damu ya Watanzania na Wana-Afrika Kusini, wakati umefika sasa kwa mahusiano hayo kuelekezwa katika nyanja ya kiuchumi kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili na hasa Watanzania.
Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wameshuhudia utiaji saini wa makubaliano katika maeneo mawili na pia wamehutubia mkutano wa waandishi wa habari.
Makubaliano yaliyotiwa saini ni ya kuanzisha ushirikiano wa jumla chini ya utaratibu mpya wa Bi-National Commission na ule wa ushirikiano katika nyanja ya utamaduni ambayo kwa upande wa Tanzania yametiwa saini na Mawaziri Benard Membe na Emmanuel Nchimbi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Kikwete amesisitiza kuwa bado nchi masikini za Afrika zinahitaji misaada, lakini misaada hiyo haihamishi wajibu wa maendeleo ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa nchi hizo. “Hatuwezi kuuacha wajibu wa maendeleo yetu mikononi mwa mtu mwingine. Huu ni wajibu wetu wenyewe.”
Kesho, Jumatano, Rais Kikwete atakwenda mji wa Cape Town ambako atakuwa na siku ya pili na ya mwisho ya ziara hiyo ya Afrika Kusini.
Mwisho.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.
19 Julai, 2011