RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Septemba 10, 2014, alifanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Museveni ambaye alikuwa kwenye ziara ya siku moja ya kikazi Tanzania, aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 4 na dakika 10 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais Kikwete.
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, yalianza saa tano unusu asubuhi na kuchukua kiasi cha saa moja na dakika 15. Rais Museveni aliondoka Ikulu baada ya chakula cha mchana na aliagana na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kabla ya kupanda ndege yake kurejea nyumbani.