Jengo la Airp Port Mkoa wa Mbeya.
Mtwara,
RAIS Jakaya Kikwete ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuuandaa mkoa huo kupokea uchumi mkubwa wa gesi na mafuta, ambao utakuja na mahitaji makubwa ya shughuli za kijamii.
Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo leo asubuhi wilayani Masasi katika kikao cha majumuisho mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi Mkoani mtwara.
Rais ameyataja matayarisho yanayohitajika ni katika bandari ya Mtwara na kuwatayarisha vijana kupokea ajira zitakazotokana na uwekezaji huo mkubwa katika gesi na mafuta.
“Mnahitaji kutengeneza mpango mkubwa wa mji kwa ajili ya kupokea changamoto za uchumi mpya wa gesi na mafuta mbali na ule mliozoea wa korosho”. Rais ameeleza.
Tayari wawekezaji wakubwa kutoka Australia, Brazil, Norway na Uingereza na wengine zaidi wanatarajiwa kuwekeza mkoani Mtwara kutokana na mali ghafi zilizoko mkoani Mtwara.
Amesema bandari ya Mtwara inahitajika kupanuliwa zaidi kuweza kuhudumia wawekezaji hao na tayari wawekezaji wamejitolea kujenga sehemu itakayoweza kuhudumia zao la korosho katika bandari hiyo.
Rais pia amewahimiza viongozi kuulea na kuusimamia mfumo mchanga wa stakabadhi ghalani kwani una mhakikishia mkulima bei nzuri na soko la mazao yake. Rais amesema serikali sasa inaanza hatua ingine ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao kwa kuibangua.
“Tukiuza korosho zetu zilizobanguliwa inaongeza thamani na tunataka thamani hii iende kwa mkulima, hili ni jambo jema likisimamiwa vizuri litakua na manufaa zaidi”. Rais amesema.
Katika ziara yake Rais ametembelea na kuona wakulima kadhaa ambao tayari wameanza kubangua korosho zao na kuziuza zikiwa katika hatua hii ambayo ina faida zaidi.
Hata hivyo amesema ili kupata mazao mazuri, huduma na pembejeo kwa zao la korosho ni muhimu sana hivyo bodi haina budi kusimamia jambo hilo kwa umakini ili pembejeo hizo zikiwemo dawa zipatikane kwa wakati.
Akiwa Mkoani Mtwara Rais ameambiwa wakulima wamepata zao lingine ambalo ni la choroko. Zao hili lina soko la uhakika nchini India lakini mwaka huu limepata tatizo la bei hapa mkoani na Rais amewataka viongozi kulisimamia na kutafuta soko la uhakika.
Amesema pamoja na hilo serikali imeanzisha bodi ingine ya mazao mchanganyiko ambayo nayo inaweza kutumika katika kutatua tatizo la soko kwa wakulima hao wapya wa choroko.
Rais amesema katika kilimo kwanza, utafiti unahitajika sana na kuanzia mwaka jana serikali imetenga pesa kwa ajili ya kuwafundisha vijana zaidi na itaendelea kufanya hivyo ili utafiti wa uhakika na vijana waliosoma na kuwa na vifaa vya uhakika waweze kuongoza na kufanya kazi ya kilimo kizuri.
Amesema mwaka huu shughuli za ukarabati wa vituo hivyo nchini kote utaanza ili vituo hivyo viwe chachu ya maendeleo katika kilimo kwanza.
Rais pia ameona tatizo kubwa la maji mkoani humu na hivyo kuwataka viongozi kutayarisha mpango kabambe wa maji kwa ajili ya wilaya za Newala, Nanyumbu, Masasi na Mtwara vijijini kama mwanzo wa kuelekea kutatua tatizo hilo kubwa katika wilaya hizi.
Rais ametembelea na kukagua miradi na vyanzo kadhaa vya maji lakini bado havitoshelezi katika wilaya hizi.
Rais amewataka viongozi kutafuta vyanzo vingine vya maji kwani mahitaji yataongezeka zaidi.
Rais amekamilisha ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara na anatarajiwa kurejea Dar es Salaam jioni ya leo.