RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha na vikao vya kulipana posho bali kwa viongozi kufanya maamuzi na kuyatekeleza haraka. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inachelewa kupata maendeleo ya haraka kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kwanza kujadili badala ya kuchukua maamuzi na kuyatekeleza.
Rais Kikwete ametoa tahadhari hiyo ya kuchelewesha maendeleo wakati alipozindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani kwenye siku yake ya tatu ya ziara ya kikazi katika Mkoa huo
Oktoba 5, 2013.
Akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli zinazofanywa na vijana 50 kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao wanajifunza mbinu na maarifa ya kilimo bora katika kambi hiyo, alitaka kujua kama makampuni mawili yaliyoomba ardhi ya kulima kisasa katika bonde la Mto Rufiji, yamepewa ardhi ya kuanza kulima.
Awali katika maelezo yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Rufiji (RUBADA), Bwana Aloyce Masanja yaliashiria kuonyesha kuwa makampuni hayo, Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings Company Limited yalikuwa yamepewa ardhi na Mamlaka hiyo kama yalivyokuwa yameomba.
Lakini Rais Kikwete alipotaka maelezo ya ziara kutaka ukweli kama makampuni hayo yamepewa ardhi na ni kiasi gani, Bwana Masanja alithibitisha kuwa Frontline Development Partners walioomba hekta 20,000 walikuwa hawajapewa hata hekta moja na kuwa Lukurilo Holdings walioomba hekta 12,000 walikuwa wamepewa 4,000 tu.
Rais Kikwete alishangazwa na hali hiyo na kusema: “Kwa miaka minne sasa tumekuwa tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi wake. Tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu, Dar Es Salaam, na kukubaliana. Imetokea nini? Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo sasa tunaendelea kujadili nini?”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nchi yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kuanza kujadili. Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala na kwa vikao vya kulipana posho visivyoisha. Hatuwezi kuendeleza nchi kwa mwenendo huu – Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima kiasi cha miaka mitano iliyopita…”
Rais Kikwete ambaye amewaamuru viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo amesema: “Nchi inakwamishwa na watu wa namna hii, kila siku kuzungumza na kujadiliana…hadithi haiishi. Maendeleo yetu yanachelewa kwa sababu mizunguko – kila siku mnazunguka, hamumalizi.”
Mapema Rais Kikwete amewaambia viongozi wa kambi hiyo ambayo inamilikiwa na RUBADA kuwa kazi ya kambi hiyo iwe ni kuandaa vijana wa kujiajiri kwa kilimo cha kisasa na siyo kuandaa watu wa kutafuta kazi ya kuajiriwa katika kilimo.
“Tunaandaa wakulima wazuri, vijana, na siyo tunaandaa kundi la watu wa kutafuta ajira ya kilimo. Hatuwezi kuwa na kambi ya namna hii ikiandaa kundi la watu wa kutafuta ajira…kijijini utaajiriwa na nani kama siyo kushiriki kilimo?”
Rais Kikwete, hata hivyo, amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi wa kuandaa vijana hao kushiriki katika kilimo kwa sababu mageuzi ya kilimo yataletwa na vijana.
“Tukiingiza vijana katika shughuli za kilimo basi mageuzi ya kilimo katika nchi yetu yanawezekana kwa sababu ni dhahiri kuwa mageuzi ya kilimo yatakuwa magumu kuletwa na baba zao, na magumu zaidi kuletwa na babu zao.”
Rais ambaye alikuwa kwenye ziara ya Wilaya ya Rufiji pia amezindua mradi mkubwa wa maji mjini Kibiti na amekabidhiwa boti ambazo zitafanya shughuli za kubeba wagonjwa katika maeneo ya Nyamisati na visiwa vya jirani.