Na Magreth Kinabo, Maelezo-Dodoma
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajiwa kulihutubia Bunge Maalum la Katiba pamoja na kulizinduwa Machi 21, 2014 mjini Dodoma. Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa bunge hilo, Yahya Khamis Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa ofisi za Bunge mjini Dodoma.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 75 (1), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atalihutubia Bunge Maalum siku ya Ijumaa Machi 21, mwaka 2014 saa 10 jioni, ambapo wageni waalikwa wote watatakiwa kuwa wameingia na kuketi katika maeneo watakayoelekezwa saa 9:00 alasiri,” alisema Katibu Hamad.
Alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza na kikao cha Bunge saa 9:10 na baadaye kikao hicho kitaanza saa 9:20 kwa ajili ya kumpokea Rais. Aliongeza kuwa mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge, Rais Kikwete atapokewa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, ambapo baadaye ataelekea katika jukwaa maalum kwa ajili ya kupokea salamu za heshima na kukagua Gwaride Maalum ambalo limeandaliwa na Jeshi la Polisi.
Alisema baada ya shughuli zote kufanyika katika viwanja vya Bunge utaratibu umewekwa kwa viongozi kuingia Bungeni kwa maandamano maalum. Viongozi watakaohusika katika maandamano hayo ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na hatimaye Rais Kikwete ambaye atafuatana na Mwenyekiti wa bunge hilo.
Katibu huyo aliwataja viongozi wegine walioalikwa kuwa ni viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu kutoka pande zote za Muungano, viongozi wa kitaifa wastaafu, ambao ni marais wastaafu kutoka pande zote za muungano, mawaziri wakuu wastaafu, waziri kiongozi mstaafu na maspika wastaafu.
Viongozi wengine ni mama Maria Nyerere, Mama Shadia Karume na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wageni wengine walioalikwa katika utaratibu huo ni taasisi za dini, taasisi zisizo za kiserikali, tasnia ya habari, vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu, vyama vya watu wenye ulemavu, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wakulima na wawakilishi kutoka sekta binafsi.
Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli hiyo Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia bunge hilo kwa muda wa saa moja. Hivyo shughuli hizo zitakamilika majira ya saa 12:00 jioni.