Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inakaribia kukamilisha ujenzi wa madaraja yote 10 yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na ambayo yanagharimu mabilioni ya fedha.
Rais Kikwete amesema kuwa kati ya madaraja hayo ambayo thamani yake inakaribia sh. bilioni 415, madaraja mawili tayari ujenzi wake umekamilika. Madaraja hayo ni lile la Ruhekei lililoko Wilaya ya Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma na Daraja la Mwatisi katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete amesema kuwa madaraja mengine saba yanaendelea kujengwa, ikiwa ni pamoja na Daraja la Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam linalogharimu sh bilioni 214.6, Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Mkoa wa Kigoma unaogharimu sh bilioni 90.185, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro linalogharimu sh bilioni 53.214 na Daraja la Rusumo, Mkoa wa Kagera linalogharimu sh bilioni 31.7.
Madaraja mengine yanayoendelea kujengwa ni Daraja la Sibiti, Singida, linalogharimu sh bilioni 17.5, Daraja la Nangoo, Mkoa wa Mtwara linalogharimu sh bilioni 4.29 na Daraja la Maligisu, Mwanza, linalogharimu sh bilioni 2.51.
Amesema Rais Kikwete: “Madaraja niliyotaja ujenzi wake ukikamilika, tutakuwa tumetimiza ahadi yetu ya kujenga madaraja yote yaliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 isipokuwa Daraja la Ruhuhu ambalo maandalizi yake ya ujenzi yanaendelea.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumza wakati anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mbutu, Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora katika sherehe ya kufanya iliyofanyika Jumatatu, Januari 7, 2013.
Rais Kikwete amesema kuwa baadhi ya madaraja yanayojengwa sasa na Serikali yalipangwa kujengwa katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo mwaka 1968 lakini kwa bahati mabaya hayakuweza kujengwa. Madaraja hayo ni Daraja la Kigamboni, Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Rufiji, Daraja la Kilombero, Mkoa wa Morogoro na Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi.
Awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu ilijenga Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Awamu na pili ikafanya maandalizi na Awamu ya tatu ikajenga Daraja la Rufiji na Awamu ya sasa inajega madaraja matatu yaliyobakia – Kilombero, Kigamboni na Kikwete.”
Daraja la Mbutu lina urefu wa kilomita tatu, na linajengwa katika Bonde la Mbutu na litaunganisha mikoa ya Tabora, Singida, Simiyu na Shinyanga.
Daraja hilo litakuwa na daraja moja kubwa la mita 60 na madaraja mengine madogo saba na hivyo kufanya urefu wa daraja lote kuwa na mita 165. Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi wa daraja hili lenye thamani ya sh bilioni 11.28 umekamilika na inakadiriwa kuwa litakuwa tayari ifikapo Novemba mwaka huu.