Na Janeth Mushi, Arusha
RAIS wa Tanzania Jakaya Kikwete kesho anatarajiwa kufungua Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa Afrika (ACBF), unaoshirikisha viongozi waandamizi katika sekta ya Fedha, kujadili namna ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana barani Afrika.
Akizungumza leo mjini hapa Waziri wa fedha, Mustafa Mkulo aliwaambia washiriki wa mkutano huo unaoshirikisha nchi 12 toka barani Afrika kuwa, kupitia utafiti uliofanywa mwaka 2006 umeonesha asilimia kubwa ya vijana hawajaajiriwa huku asilimia 80 wakiwa sekta isiyo rasmi.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkulo, Kamishna wa Fedha za
Nje kutoka Wizara ya Fedha, Ngosha Magonya, alisema kutokana na hali hiyo kuna changamoto kubwa kuharakisha maendeleo, ikiwa ni
harakati za kuimarisha uchumi barani Afrika.
Aidha alishauri kufanyika mbinu za kubuni ajira kwa vijana jambo ambalo litachangia kupunguza ukubwa wa tatizo. Mkutano huo unawakutanisha mawaziri wa fedha na wataalamu wa mambo ya uchumi watakaojadili matumizi ya fedha za misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali.
Alisema wataalamu hao watashiriki mkutano huo ambao unafanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza tangu ACBF ilipoundwa miaka 20 iliyopita watajadili program za maendeleo zinazosimamiwa na umoja wa mataifa (UN) kwenye nchi zao.
Kamishna huyo alisema kuwa jambo lingine litakalojadiliwa katika
mkutano huo ni pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana barani
Afrika ambapo kwa hapa nchini limeonekana kuwa janga la kitaifa.
Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi wa ACBF, Dk. Frannie
Leautier alisema kuwa lengo la Taasisi hiyo ni kuhakikisha fedha
zinazotolewa na wahisani katika nchi za Afrika ikiwemo Benki ya Dunia
zinatumika ipasavyo.
Frannie alisema lengo la kukutana na magavana hao pamoja na
wataalamu wa masuala ya fedha ni kuhakikisha wanajadili kwa kina
matatizo sugu yanayozikumba nchi zao na kuibadilishana uzoefu kwa
lengo la kutatua changamoto zinazowakabili. Katibu huyo alisema mkutano huo unatarajiwa kusaidia kuboresha ubunifu na utekelezaji wa sera utakaoleata matokeo endelevu za nchi mwanachama.
Katika mkutano huo wa siku tatu wasemaji wakuu ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi, Mipango na Uchambuzi wa Sera kutoka Benin, Marcel de Souza, Waziri Mkuu mstaafu wa Mauritania, Zeine Ould Zeidan watakaoongoza mjadala juu ya changamoto za ajira kwa vijana barani Afrika na hatua zinazotakwia kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.
Aidha Mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo Afrika (ADI), Victor Murinde
na mkurugenzi wa sera za uchumi pamoja na mshauri wa utawala bora wa Benki ya Dunia, Deryck Brawn wataongoza mjadala kuhusu viashiria vya uwezo wa Afrika kuelekea mkutano wa Busan nchini Korea Kusini unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.