JK: Kifo cha Osama ni unafuu kwa walioumizwa

Osama bi Laden

Na Edson Kamukara
Dar es Salaam

RAIS Jakaya Kikwete amesema kifo cha Kiongozi wa kundi la Al-qaeda, Osama Bin Laden kitaleta unafuu na kuwapunguzia machungu watu waliopoteza ndugu zao ama kujeruhiwa katika matukio yaliofanywa na kundi hilo wakiwemo Watanzania.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la mwandishi wa habari kwenye mkutano wa Tume ya Shirika la Umoja wa Mataifa (WHO) uliyokuwa ukijadili uboreshaji wa afya ya uzazi wa wananwake na watoto.

Mwandishi huyo, alitaka kujua kauli ya Tanzania baada ya Marekani kutanganza kumuua kiongozi huyo usiku wa kuamkia jana, kwa vile ilikuwa ni moja ya mataifa yaliyopoteza raia wake katika shambulio la kigaidi lililofanywa kwenye Ubalozi wa Marekani nchini.

Akijbu swali hilo, Rais Kikwete alisema si vyema kushangilia kuuawa kwa mtu mwingine kwa vile ni kinyume na matwaka na haki za binadamu, lakini akalitaja shambulio hilo la Agosti 7, 1998 kuwa lilileta majonzi makubwa.

“Watu 11 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa na baada ya hapo uchunguzi ulianza ambapo watuhumiwa kadhaa walikamatwa akiwemo Mtanzania aliyekamatwa nchini Pakstani. Lakini vidole vyote lilinyooshewa kundi la Al-qaeda”

“…Lakini leo (jana) tumesikia Osama kauawa. Mimi ninaloweza kusema katika hilo ni kwamba pengine hatua hiyo italeta relief (ahueni) kwa Watanzania waliopoteza ndugu na jamaa zao katika shambulio hilo la kigaidi,” alisema Rais Kikwete.

Shambulio hilo la kigaidi jijini Dar es Salaam katika Ubalozi wa Marekani mwaka 1998 lilifanyika kwa muda mmoja na lile la jijini Nairobi nchini Kenya saa nne asubuhi ambapo pia Ubalozi wa Marekani nchini humo ulilipuliwa na watu wengi kupoteza maisha.