Na Joachim Mushi
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kutolewa kwa adhabu mbadala na mahakama kutapunguza msongamano mkubwa wa wafungwa gerezani, hivyo kuishauri taasisi hiyo nyeti ya sheria kuanza kufikiria adhabu mbadala kwa wahalifu.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Tanzania.
“Hatuna budi kutumia adhabu mbadala kama sheria ya The Community Act inavyoruhusu kwa makosa yanayostahili. Sheria hiyo inajenga dhana kwamba jukumu la kuwarekebisha wahalifu haliko mikononi mwa Serikali pekee na kwamba jamii wanakotoka wahalifu nayo ina wajibu wa kushiriki katika kuwarekebisha wahalifu,” alisema Rais Kikwete katika hatuba yake.
Aidha alikiri kuwa mfumo wa sasa wa adhabu unasisitiza adhabu ya kifungo jela badala ya adhabu mbadala ambazo zipo katika sheria na kuongeza kwamba kama adhabu mbadala zingekuwa zinatolewa, idadi ya wafungwa gerezani ingepungua na hata tatizo la msongamano katika magereza lisingekuwepo au lingepungua sana.
Alisema sheria ya kufanya kazi ya kijamii ililenga kuwaepusha na adhabu ya kifungo wale wafungwa ambao wameonesha tangu awali waliteleza, wametubu na kuomba msamaha, japokuwa alisema utekelezaji wa sheria hiyo una changamoto zake.
Akizitaja moja ya changamoto hizo, Rais Kikwete alibainisha jamii ina kila sababu ya kukubali ukweli kwamba wahalifu wanarekebishika, na kwamba adhabu zinazotolewa zina lengo la kumrudi na kumrekebisha mhalifu.
“Inapodhihirika kuwa mwenendo wa mhalifu una muelekeo mzuri na hasa unapopima uzito wa kosa alilofanya ni dhahiri kwamba ni kwa manufaa ya mfungwa kurekebishwa na jamii badala ya kumtenga kwa kumfunga gerezani. Hii ni namna nyingine ya kumpa mhalifu fursa ya kujirekebisha katika jamii yake.” Anasema Rais Kikwete.
Hata hivyo alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othuman kwa mada nzuri ya maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka huu inayosema “Adhabu Mbadala Katika Kesi za Jinai na Faida zake katika jamii” na kuongeza kuwa ni ujumbe ambao umekuja wakati muafaka na muhimu.
Aidha changamoto zingine ambazo aliziainisha ni pamoja na jamii kutambua na kukubali kuwa inao wajibu mkubwa katika kusaidia kuwarekebisha wahalifu, kwani hadi sasa upo ugumu kwa jamii kulielewa jambo hili hivyo wengi kuamini kwamba adhabu pekee ya mhalifu ni kumfunga gerezani.
“…Ipo kazi kubwa ya kutoa elimu ili watu nao waelewe kuwa wanao wajibu wa kusaidia kuwarekebisha wafungwa wawe na tabia njema. Changamoto nyingine ni jinsi jamii itakavyojipanga kufanya kazi ya kuwarekebisha wahalifu katika jamii zao. Ingefaa wadau muhimu, kama vijiji, Halmashauri na Mamlaka nyingine wabuni kazi na kutenga
maeneo ya kufanya kazi zenye manufaa kwa umma,” alisema.
“Ni muhimu kwa ajili hiyo basi, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa wakahusishwa kwa ukamilifu katika utekelezaji wa adhabu mbadala. Tukifanya hivyo mpango huu utakuwa umepewa msukumo wa pekee na kupata mafanikio,” aliongeza katika hatuba hiyo.
Aidha, alimpongeza Jaji Mkuu, Othuman kwa kuuongoza vema mhimili wa Mahakama kwani ameufanya kuwa daraja imara kati ya mihimili mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Alisema chini ya uongozi wa Jaji Mkuu huyo mafanikio mengi yamepatikana na heshima na taswira ya Mahakama katika jamii inazidi kuboreka.
“Nakushukuru sana. Nawapongeza, pia, Majaji wa Rufaa, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu pamoja na watumishi wengine wote wa Mahakama. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa na nzuri pamoja na kuwepo changamoto mbalimbali.,” alisema Kikwete.