Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Morogoro Onesphory Mkude, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga Anthony Banzi, viongozi wa mkoa wa pwani na kamati ya walei ya Parokia ya Lugoba, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Oktoba 27, 2013 wakati wa sherehe za Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia hiyo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Morogoro Onesphory Mkude, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga Anthony Banzi, viongozi wa mkoa wa pwani wakati wa sherehe za Jubilei ya Miaka 100 ya Parokia hiyo.
HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO W A TANZANIA KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 100 YA KANISA KATOLIKI, PAROKIA YA LUGOBA, TAREHE 27 OKTOBA, 2013
Mhashamu Baba Askofu, Telesphor Mkude, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro;
Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga;
Wahashamu Maaskofu,
Viongozi wa Dini mliopo hapa;
Baba Paroko, Padri Constantine Luhimbo;
Mapadri, Mashemasi na Watawa;
Ndugu waumini;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani kwa Mwaliko
Niruhusuni niungane na wasemaji walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutukutanisha hapa katika Kanisa la Msalaba Mtukuka kusherehekea Jubilei ya miaka mia moja ya Kanisa Katoliki la Lugoba. Nakushukuru sana Baba Askofu Mkude pamoja na Baba Paroko na waumini wa Parokia ya Lugoba kwa kunishirikisha katika maadhimisho haya ya kihistoria.
Nawapongeza sana waumini wa Parokia ya Lugoba kutimiza karne moja tangu ianzishwe. Hayo ni mafanikio makubwa, hivyo mnastahili kusherehekea kwa nderemo na vinubi. Nawapongeza sana kwa kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwashukuru Padri Cornel na Padri Herman ambao ndiyo waanzilishi wa Parokia hii miaka 100 iliyopita. Hakika leo ni siku yao wao zaidi pengine kuliko sisi. Bila ya juhudi zao, moyo wao wa ujasiri, uvumilivu na kujituma huenda leo tusingekuwa hapa kufanya maadhimisho haya. Sote tumesikia kuwa mwanzoni mambo hayakuwa rahisi sana. Lakini, ni ushirikiano wa Wamisionari hao na baadhi ya wenyeji kama vile Mzee Kinogile, aliyekuwa Mtawala, Mzee Matei, Mzee Lui na wengineo ndiyo weliowezesha mambo kwenda vizuri na Parokia ikaanzishwa. Nafurahi nao pia mmewatambua na kuwaenzi.
Kwa ujumla nimefarijika sana kuona kwamba katika kusherehekea siku ya leo mnawatambua na kuwaenzi watumishi wa Mungu tangu wakati ule mpaka sasa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kujenga na kuimarisha kanisa kwenye Parokia hii. Kutokana na kazi yao nzuri waumini wameongezeka, huduma za kiroho zimeimarika na kwamba Kanisa limetoa mchango muhimu kwa maendeleo ya jamii katika eneo letu hili.
Ndugu waumini;
Ninyi na mimi ni shuhuda wa jinsi Kanisa Katoliki la Lugoba lilivyochangia na linavyoendelea kuchangia katika upatikanaji wa huduma za jamii kama vile elimu na afya bila ya kuwabagua watu kwa imani zao za kumuabudu Mungu. Kwa upande wa afya tumesikia zahanati zilizojengwa na Kanisa na mipango iliyopo ya kuboresha zaidi huduma zinazotolewa. Vile vile, tumesikia shule zilizojengwa na kuanzishwa na Kanisa la Lugoba. Hata mimi ni mmoja wa watu walionufaika kwani nilipata elimu ya darasa la tano hadi la nane mwaka 1962 mpaka 1965 katika shule iliyokuwa inaitwa St. John Bosco’s Lugoba Middle School iliyomilikiwa na Kanisa Katoliki Lugoba.
Kunako mwaka 1965, Serikali iliamua kuwa elimu za msingi hazitakuwa na madaraja mawili yaani ya darasa la kwanza hadi la nne (Primary School) na darasa la tano hadi la nane (Middle School) badala yake elimu ya msingi ikawa kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. Kufuatia uamuzi huo Lugoba Middle School na Lugoba Primary School ziliunganishwa na kuwa shule ya Msingi Lugoba. Wakati madarasa tuliyosomea yanaunganishwa na shule hiyo mpya, iliyokuwa ofisi ya Walimu ikawa zahanati ya Kanisa na yaliyokuwa mabweni sasa yamekuwa madarasa ya Sekondari ya Lugoba.
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuzindua zahanati katika Parokia ya Lugoba, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Oktoba 27, 2013 wakati wa sherehe za Jubilei ya Miaka 100 wa Parokia hiyo ya Miaka 100 wa Parokia hiyo.
Mke wa Rais Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya watawa katika Parokia ya Lugoba, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Oktoba 27, 2013 wakati wa sherehe za Jubilei ya Miaka 100 wa Parokia hiyo.i ya Miaka 100 wa Parokia hiyo. (PICHA NA IKULU).
Kwa kweli hatuna maneno mazuri ya kuelezea shukrani zetu kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Lugoba kwa mchango muhimu iliyotoa kwa maendeleo ya watu wa eneo hili, Wilaya ya Bagamoyo na kwingineko nchini. Watu wengi wamefaidika na wanaendelea kunufaika. Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki ili muendelee kuwahudumia watu katika Parokia yetu ya Lugoba na taifa kwa ujumla. Tunapenda miaka mia moja ijayo, kwa watakaokuwepo kipindi hicho, wakiri utume huo usiokifani. Na waseme “hakika wenzetu waliotangulia walikuja kufanya kazi, walikuwa watu wa kazi”.
Serikali Inathamini Mchango wa Kanisa
Mhashamu Baba Askofu Mkude;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuwahakikishia kuwa serikali inatambua vyema na kuthamini mambo yote mazuri yanayofanywa na Kanisa Katoliki. Kabla na hata baada ya uhuru, Kanisa limekuwa mdau muhimu na mshirika muhimu wa Serikali katika kuhudumia wananchi. Wakati mwingine unakuta huduma za jamii kama zahanati ipo mahali ambapo hata Serikali bado haijafika. Kutuunga mkono kwa namna hiyo ndiko kumechangia sana nchi yetu kupiga hatua kubwa kwenye kufikisha huduma kwa jamii nchini.
Ahadi yangu kwenu ni kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu mengine ya dini kuboresha maisha ya Watanzania. Tutaendelea kupokea ushauri wenu na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naomba muendelee kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi. Muendelee kutumia mtandao wenu mpana uliopo nchi nzima kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Lengo letu libaki kuwa moja daima na milele. Tufanye kazi pamoja ili tufanikiwe zaidi.
Maombi kwa Viongozi wa Dini
Mhashamu Baba Askofu Mkude, Baba Paroko na viongozi wa dini mliopo;
Naomba muongeze juhudi za kuhubiri umoja na kutoa mafundisho ya kuhimiza udugu na mshikamano miungoni mwa Watanzania. Sote tunafahamu kuwa kuna baadhi ya watu wanaofanya juhudi usiku na mchana kuuvuruga upendo, umoja na mshikamano wa wananchi wa Tanzania. Kwa sasa watu hawa hawajafanikiwa lakini tuelewe kuwa hawajachoka na wala hawajaaacha. Wana sifa ya ushetani, maana shetani hachoki wala hakati tamaa katika kuwashawishi wanaadamu kutenda maovu. Na, hawa si ajabu wakathubutu tena na tena. Inatupasa na sisi pia tuwe macho. Naomba msilegeze uzi katika kuwaelimisha waumini wenu waelewe nia mbaya za watu wasioitakia mema nchi yetu, wawaepuke wala wasiwasikilize. Tudumishe upendo, umoja na mshikamano wetu. Sisi sote Mungu wetu ni mmoja kwa nini tuchukiane, tubaguane na hata tuuane kwa sababu ya kutofautiana katika kumuabudu Mungu? Wengine ni ndugu wa damu kwa nini tufarakane kwa namna ya kumsujudia Muumba wetu? Kila mtu aachwe kufuata dini anayoipenda na udugu wetu na umoja wetu kama wanadamu ubaki pale pale. Ipo hatari hata ndugu wa damu tukafarakana kwa sababu ya kuwa dini mbalimbali. Siyo sawa.
Niliwahi kusema siku za nyuma na leo narudia tena kuwa viongozi wa dini wanayo nafasi ya pekee katika kufikisha ujumbe huo kwa watu wote. Hii inatokana na ule ukweli kwamba wanasikilizwa na kuaminiwa sana na waumini wao na watu wengine pia. Wanasikilizwa na watu wengi. Waumini wakielezwa, wakaelewa na wote wakazingatia kuishi kama mafundisho ya viongozi wao, nchi yetu itabaki salama. Hakuna mtu atakayefanikiwa kutufarakanisha na kuichezea amani yetu. Hata kama ni muumini wa dini ya shetani.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Morogoro Onesphory Mkude, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga Anthony Banzi, viongozi wa mkoa wa pwani na kwaya pamoja na watoto wa shule ya Jumapili katika Parokia ya Lugoba, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, leo Oktoba 27, 2013 wakati wa sherehe za Jubilei ya Miaka 100 Parokia hiyo.
Pili, naomba tuendelee kusaidiana kulea nchi yetu kimaadili. Hakuna siri kwamba kuna mmonyoko mkubwa wa maadili mema. Vitendo viovu na mambo yasiyoipendeza jamii na yasiyompendeza Mwenye Mungu yanazidi kuongezeka kwenye jamii. Mambo ambayo siku za nyuma yalikuwa nadra sana kutokea au kusikika sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana ati ndiyo usasa. Matumizi makubwa ya dawa za kulevya, ngono, ubakaji, watoto kutokuheshimu wakubwa, wazee kutokujiheshimu, ulevi wa kupindukia, vitendo vya rushwa, uvivu, wizi na idadi kubwa ya ndoa kuvunjika ni vielelezo dhahiri vya hali mbaya ya kimaadili inayokabili jamii zetu nchini.
Kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na taifa kwa ujumla. Kunachangia sana kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Kunaifanya kazi ya kuondoa umaskini kuwa ngumu na kuongeza watoto wa mitaani. Kunachangia kuenea kwa maambukizi ya UKIMWI. Kunaongeza uhalifu wa aina mbalimbali nchini pamoja na mauaji.
Mimi naamini kwa dhati kuwa watu wakishika mafundisho ya dini, wakamuogopa Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua. Hayawezi kuisha kabisa lakini yatapungua sana. Ndiyo maana narejea ombi langu ninalolitoa mara kwa mara kwa viongozi wa dini zote. Tusaidiane kulea taifa letu kimaadili. Tuweke mkazo zaidi kwa vijana kwa sababu, kwanza wao ndio walengwa wakuu wa maovu yanayotendeka. Lakini pili, wao ndio taifa la leo na kesho, ndio warithi wa taifa letu. Tukiwaandaa vyema, mustakabali wa taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama. Tukishindwa leo, tutalia na kusaga meno kesho. Taifa letu litakuwa mashakani.
Mwisho
Kwa kumalizia nawapongeza wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kuandaa sherehe hizi. Kwa kweli zimefana sana na watu wote hapa ni mashahidi. Nakushukuru kwa mara nyingine tena Mhashamu Baba Askofu na Baba Paroko kwa uongozi wenu uliotukuka. Nimefurahi sana kujumuika nanyi katika maadhimisho haya. Naomba tuendelee kushirikiana kuleta maendeleo zaidi kwenye Parokia yetu na nchi yetu kwa ujumla. Tukiunganisha nguvu zetu, daima ushindi utapatikana. Naomba tuamue kuwa washindi. Tumsifu Yesu Kristu.
Asante kwa kunisikiliza.