JK: Baadhi ya Vyama vya Ushirika ni Mkusanyiko wa Wezi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifungua pazia kuzindua rasmi jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Julai 25, 2013

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa baadhi ya vyama vya ushirika nchini ni mkusanyiko wa wezi wanaokula fedha za wananchi bila hata kunawa.

Aidha, Rais Kikwete amevitaka vyama vya ushirika nchini kuacha mwelekeo wa kuwa wachuuzi tu wa kununua na kuuza tu mazao ya wananchi na badala yake vijiingize katika shughuli za uwekezaji na maendeleo ya kweli kweli ya wanachama wao.

Rais Kikwete ameyasema hayo Jumatano, Julai 24, 2013, wakati alipozungumza na wananchi baada ya kufungua jengo la kitega uchumi la Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU) mjini Bukoba.

Rais Kikwete amewaambia wananchi waliokusanyika kwenye tukio hili, “Hapa Kagera ni kitovu cha ushirika. Na KCU ni kitovu cha kuboresha na kuleta usasa katika shughuli za ushirika. Siyo kama vyama vingine ambavyo ni mkusanyiko wa wezi wanaokula wazi wazi mchana bila hata aibu ….wanakula bila kunawa.”

Baada ya kuwa ameelezwa mafanikio makubwa ya KCU na shughuli za ushirika katika Mkoa wa Kagera, Rais Kikwete ameongeza: “Sasa kama siyo mkusanyiko wa wezi ni nini? Huko nyuma Serikali yenu ilifanya uamuzi wa kulipa madeni yote ya ushirika nchini ili kuvipunguzia vyama mzigo wa kujiendesha. Lakini sasa vyama hivyo hivyo vimeanza kujitumbukiza tena katika madeni kwa sababu katika baadhi ya vyama hivi hakuna viongozi waaminifu wala waadilifu.”

Kuhusu shughuli za ushirika kwa jumla, Rais Kikwete ametaka vyama vya ushirika sasa kuachana na ulanguzi wa kununua na kuuza mazao ya wakulima na badala yake vyama hivyo vijiingize katika maendeleo ya kweli kweli ya wanachama wao.

“Tuachane sasa na kazi ya ulanguzi. Tusiwe wachuuzi tu wa kununua na kuuza mazao ya wakulima. Tujiingize katika maendeleo ya wanachama wetu kwa kuwekeza kama kinavyofanya chama chetu cha KCU,” amesema Rais Kikwete.

Amekipongeza KCU kwa jengo jipya la kitega uchumi na akataka vyama vingine kuiga mfano wa chama hicho siyo tu katika uwekezaji bali hata katika kuleta mabadiliko na usasa katika shughuli za ushirika.

“Mnajua ushirika kwetu hapa nchini umepitia katika historia ya matatizo. Mabadiliko mengine ya sera yametufikisha hapa tulipo na tunalazimika kuunda na kuujenga upya ushirika wetu nchini. Kazi hii ya kujenga upya, hata hivyo, inaweza kufanywa na viongozi waadilifu na waaminifu.”

Rais amesisitiza kuwa lengo kuu la vyama vya ushirika liwe ni kutetea maslahi ya wanachama wao na kwa Kagera lengo liwe ni kutetea wakulima wa kahawa na shughuli zote za utendaji wa KCU zilenge huko.

Jengo hili la ghorofa la kitega uchumi limejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 1.1 na litakuwa na ofisi, hoteli na maduka ya biashara.

Kabla ya kuzindua jengo hilo, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi kwenye Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba ambao unapanuliwa na kufanywa wa kisasa kwa gharama ya Sh. bilioni 21.015.

Mradi huo wa upanuzi ulianza Februari, mwaka jana, na unatarajiwa kukamilika Februari mwakani na upanuzi huo ukikamilika Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wasafiri 500,000 kwa mwaka sawa na wasafiri 150 kwa saa.

Akizungumza kwa ufupi tu baada ya kuweka jiwe hili la msingi, Rais amesema: “Kwa kupanua Uwanja huu, tumetimiza ahadi yetu. Tuliahidi kuwa tutapanua Uwanja huu na sasa tumetekeleza.”

Lakini Rais Kikwete ameongeza: “Lakini hii ni ahadi moja. Ahadi yetu nyingine ya kujenga uwanja wa kimataifa kule Omukajunguti bado iko pale pale. Upanuzi wa Uwanja wa Bukoba ni hatua ya muda tu wakati tunajiandaa kuanza ujenzi wa ule mkubwa zaidi.”

Rais Kikwete amewasili mjini Bukoba mchana wa leo kuanza ziara ya siku sita katika Mkoa wa Kagera ambayo itampitisha katika wilaya zote za Mkoa huo.