Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Februari 27, 2014, amezindua Mtambo wa Kuhakiki na Kusimamia Mawasiliano ya Simu (Telecommunications Traffic Monitoring System –TTMS) katika sherehe fupi lakini ya kufana iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mjini Dar Es Salaam.
Mtambo huo unalenga kuhakiki na kusimamia mawasiliano ya simu zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi kwa kubaini jinsi matumizi ya simu yanavyofanyika, kubaini bei zinazotozwa na faida inayopatikana pamoja na kuihakikishia Serikali mapato yake stahiki.
TCRA imeupata mtambo huo wenye gharama ya dola za Marekani milioni 25 bila kuununua moja kwa moja. Mtambo huo umenunuliwa na kufungwa na Kampuni ya SGS ya Uswisi ikishirikiana na Kampuni ya JVG ya hapa nchini. Kampuni hiyo itausimamia na kuuendesha mtambo huo kwa miaka mitano chini ya utaratibu wa “Jenga, Endesha na Hamisha – Build, Operate and Transfer” kipindi ambako itaweza kurudisha gharama zake kabla ya kuukabidhi kwa TCRA.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma amemwambia Rais Kikwete katika sherehe hizo kuwa ufungaji wa mtambo huo hautaongeza bei ya mawasiliano kwa watumiaji wa simu. Badala yake, amesema Profesa Nkoma, Serikali itanufaika kwa kupata kiasi cha dola za Marekani milioni moja kwa mwezi ikiwa ni gawio lake kutokana na faida itakayotokana na mtambo huo mpya.
Tayari TCRA imekwishakabidhi kwa Serikali dola milioni moja za mwezi uliopita na katika sherehe, Profesa Nkoma ameikabidhi Hazina mfano wa hundi yenye thamani ya sh. 1,684, 357. 283 (sawa na dola milioni moja) kwa mwezi wa Februari. Amesema kuwa fedha yake tayari imewekwa kwenye Akaunti ya Mfuko wa Hazina.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano katika miaka tisa iliyopita na jinsi gharama za mawasiliano zilivyopungua katika kipindi hicho kutokana na hatua mbali mbali zilizochukuliwa na serikali na hasa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa.
Amesema kuwa matumizi ya simu yameongezeka kutoka laini za simu milioni 3.6 mwaka 2005 hadi kufikia laini milioni 28 mwishoni mwa mwezi uliopita wakati watumiaji wa Internet wameongezeka kutoka milioni 4.9 mwaka 2011 hadi kufikia milioni tisa wa sasa.
Kuhusu gharama za simu, Rais amesema kuwa gharama hizo zimepungua kwa asilimia 57 kati ya mwaka 2009 na 2013 kwa upande wa simu wakati punguzo hilo kwa upande wa internet.