Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal akiwasili katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Mawasiliano ya Intaneti. |
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal (wa pili kushoto) akipata maelezo namna kituo cha mawasiliano ya intaneti cha TTCL kilichozinduliwa leo kinavyotoa huduma zake. |
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal akibofya kitufe kuzinduwa rasmi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. |
Salamu za shukrani kwa mgeni rasmi toka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia zikitolewa na Katibu Mkuu. |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete leo amefanya uzinduzi wa Kituo cha Mawasiliano ya Intaneti (Internet Protocal Point of Presence-IP POP) cha Kampuni ya Simu nchini Tanzania (TTCL), tukio ambalo amelifanya leo Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akimuwakilisha Rais Kikwete.
Tukio hilo limefanyika leo jijini Dar es Salaam pamoja na lile la kuzinduwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ikiwa ni juhudi za Serikali, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na Kampuni ya Simu nchini Tanzania (TTCL) kuboresha huduma za mawasiliano nchini na nchi za jirani zinazohudumiwa na Tanzania.
Akizungumzia kituo cha ‘IP POP’, Dk. Bilal aliipongeza kampuni ya Simu Tanzania TTCL kwa kujenga kituo cha kisasa cha kimataifa cha mawasilino ya intaneti nchini ambacho kitasaidia kutoa huduma bora za mawasiliano pamoja na kupunguza gharama za mawasiliano hayo. Kituo cha ‘IP POP’ kimejengwa pia kwa ubia na kampuni ya Telekom Italia Sparkle (TIS) kwa ushirikiano na TTCL.
“…Kituo hiki ni muhimu kwa maendeleo ya sekta na kwa hakika kitasaidia kuboresha utoaji wa huduma za intaneti kwa gharama nafuu hapa nchini na katika nchini za Afrika Mashariki na zile za ukanda wa Maziwa Makuu,” alisema Dk. Bilal katika hotuba yake.
Alisema kituo hicho cha intaneti kinalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano ya intaneti katika nchi za Afrika Mashariki na Ukanda wa Maziwa Makuu, pia kuijengea uwezo kampuni ya TTCL kuhimili ushindani katika soko kwa kuboresha huduma kila uchao.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura akizungumza katika uzinduzi huo alisema kituo walichokijenga (IP POP) kina uwezo mkubwa kiufanisi kwani kinaweza kuwasiliana na vituo vingine takribani 122 vinavyomilikiwa na Telekom Italia Sparkle kwenye nchi 28 na zaidi ya vituo 1,000 vya washirika kote duniani.
Dk. Kazaura alisema kituo hicho kinaweza kumuunganisha mteja na huduma anayoifuata kwenye mtandao wa intaneti moja kwa moja bila kupitia kwa watoa huduma wengine hivyo kupunguza urefu wa njia za mawasiliano kwa mteja kufikia maudhui.
“…Kabla ya ujenzi wa kituo hiki, TTCL imekuwa ikitoa huduma zake za mawasiliano intaneti kupitia kwa watoa huduma wengine walioko barani Ulaya. mpaka sasa katika kituo hikitayari watoa huduma za mawasiliano katika nchi za malawi, uganda, Burundi, Rwanda na watoa huduma wengine wa nchini,” alisema Dk. Kazaura.