RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewatumia rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Damian Lubuva, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana na Jumuia ya Dawoodi Bohra Tanzania kufuatia misiba iliyowapata nyakati tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka kurugenzi ya mawasiliano Ikulu leo; Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Jumuia ya Dawoodi Bohra Tanzania kufuatia kifo cha Kiongozi wa Kiroho wa Jumuia hiyo duniani, Dk. Seydna Mohammed Burhanuddin ambaye amefariki dunia Januari 17, 2014.
Dk. Seydna Mohammed Burhanuddin, Kiongozi wa Jumuia ya Dawoodi Bohra kwa miaka 39 iliyopita, amefariki dunia nyumbani kwake katika kasri ya Saifee Mahal, eneo la Mahabar, kusini mwa jiji la Mumbai, India, kwa ugonjwa wa moyo akiwa na umri wa miaka 102.
Katika salamu zake kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Dawoodi Bohra katika Tanzania, Sheikh Tayabali Sheikh Hamzabhai Patanwalla, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Dk. Seydna Mohammed Burhanuddin, Kiongozi wa Kiroho wa Jumuia ya Dawoodi Bohra duniani kwa miaka mingi ambacho nimejulishwa kimetokea subuhi ya leo nyumbani kwake mjini Mumbai, India.”
Rais kikwete amesema: “Seydna Mohammed Burhanuddin alikuwa kiongozi mwenye busara na kiongozi bora wa kiroho ambaye katika maisha yake yote alilenga siyo kutoa uongozi wa kiroho kwa Jumuia yake ya Dawoodi Bohra bali kuunganisha madhehebu na dini nyingine duniani kwa nia ya kuhakikisha kuwa waumini wa dini mbali mbali wanaishi kwa amani na upendo, na kwa kuvumiliana hapa duniani.”
“Nilimjua binafsi Dk. Seydna Mohammed Burhanuddin na mara ya mwisho alipotembelea Tanzania nilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza naye ambako nilizidi kujiridhisha kuwa huyu alikuwa ni kiongozi mwenye sifa za ziada siyo tu katika uongozi wa kidini lakini pia katika uongozi wa kijamii.”
Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mwenyekiti wa Jumuia ya Dawoodi Bohra nchini Sheikh Tayabali Sheikh Hamzabhai Patanwalla salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mzee wetu huyu. Na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu kwa wana-Jumuia nzima ya Dawoodi Bohra hapa nchini kwetu na popote duniani. Wajulishe kuwa naungana nao katika msiba huu mkubwa. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu Seydna Mohammed Burhanuddin. Amina.”
Rais Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi pia Jaji Mstaafu na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Damian Zefrin Lubuva kufuatia kifo cha Mke wake, Mama Martha Peter Lubuva kilichotokea tarehe 17 Januari, 2014 katika Hospitali ya Apollo iliyoko New Delhi nchini India alikopelekwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mke wako, Mama Martha Peter Lubuva aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Apollo nchini India akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari ambao umesumbua kwa muda mrefu”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema anatambua fika machungu ambayo hivi sasa wanapitia watoto na Familia nzima ya Mheshimiwa Damian Zefrin Lubuva kutokana na kuondokewa na Mama yao Mzazi na Kiongozi muhimu wa Familia, lakini amewaomba wawe watulivu na wavumilivu, lakini muhimu zaidi wawe na moyo wa ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.
“Ninawahakikishia kuwa niko pamoja nayi katika kuomboleza msiba huu mkubwa na namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Mama Martha Peter Lubuva kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola”.
Aidha katika Salamu za Rambirambi kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Kinana kufuatia kifo cha Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali, Deusdedith Makandila Mtambalike aliyefariki dunia tarehe 16 Januari, 2014 nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Alisema enzi za Uhai wake, Marehemu Deusdedith Mtambalike, licha ya kuwa Kada hodari wa CCM, aliwahi kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya za Ngara na Muleba Mkoani Kagera, Wilaya ya Igunga katika Mkoa wa Tabora, Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Iringa na katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Deusdedith Makandila Mtambalike, Kada makini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mmoja wa Viongozi makini katika Utumishi wa Umma aliyewahi kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali hapa nchini”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Desudedith Mtambalike, enzi za uhai wake, kama Kada Hodari, Mwaminifu na Mchapakazi wa Chama Cha Mapinduzi, na mmoja wa Wakuu wa Wilaya aliyekuwa makini katika kazi zake ambaye aliutumikia wadhifa huo kwa umakini na uaminifu mkubwa, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Wananchi katika sehemu zote alizofanya kazi.
“Kuondoka kwa Mheshimiwa Deusdedith Mtambalike ni pigo kubwa kwa Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako mchango wa mawazo na ushauri wa Marehemu ulikuwa bado unahitajika sana kwetu sote”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana Salamu zangu za Rambirambi kutokana na kifo cha Kada huyu wa CCM, na kupitia kwako kwa Wanachama na wapenzi wote wa Chama Cha mapinduzi kwa kuondokewa na mwenzao, Bwana Deusdedith Makandila Mtambalike”, amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete amemuomba Kinana kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Mtambalike kwa kuondokewa na Baba, Kiongozi na Mhimili wa Familia. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao, huku akiwahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi, Roho ya Marehemu Deusdedith Makandila Mtambalike, Amina.