JK Awashukuru Watanzania kwa Upendo…!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza alipotembelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman pamoja na ujumbe wake (hawapo pichani) waliopomtembelea na kumjulia hali.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza alipotembelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman pamoja na ujumbe wake (hawapo pichani) waliopomtembelea na kumjulia hali.

RAIS Kikwete amewashukuru wananchi kwa salamu za upendo za kumtakia nafuu wakati akiwa anaendelea na matitabu yake nchini Marekani. Rais Kikwete, ambaye Novemba 12, 2014, alitoka wodini katika Hospitali ya Johns Hopkins na kuhamishiwa kwenye Hoteli Maalum jirani na hospitali hiyo, amesema ameguswa na kufarijika kwa maelfu ya salamu anazopokea kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kupitia namba maalumu ya kuwasiliana naye.

“Kwa kweli nimeguswa, nimefarijika na kutiwa moyo sana, sana kwa salamu za upendo za kunitakia heri nipate nafuu haraka pamoja na dua za wananchi kutoka kila kona ya nchi na kila pembe ya dunia”.
“Sina cha kuwalipa zaidi ya kusema tafadhalini pokeeni shukurani zangu nyingi sana kwa salamu hizo za upendo,” alisema Rais Kikwete.

Pia ametoa shukurani nyingi kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi mbalimbali, ambao nao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa kumpa pole kwa njia mbalimbali.
Rais Kikwete amekuwa akipokea takriban ujumbe mfupi kiasi cha 1,200 kwa siku toka alipotoa namba yake maalum ya simu (+1-646-309-2295), ambapo wananchi wanawasiliana naye moja kwa moja kwa njia ya ujumbe mfupi ama SMS.