JK Awaonya Maafisa TAMISEMI,Bodi ya Barabara na Wadau

Rais Kikwete akizungumza na Maafisa wa Tamisemi,Bodi ya Barabara na Wadau wa Barabara katika hotel ya Gurdoto Arusha

Rais Kikwete akizungumza na Maafisa wa Tamisemi,Bodi ya Barabara na Wadau wa Barabara katika hotel ya Gurdoto Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa niwajibu wa Mikoa na serikali za Mitaa kusimamia changamoto na mapungufu katika usimamizi wa ujenzi wa barabara nchini kama vile kuwepo kwa tuhuma za rushwa katika utoaji wa kazi za barabara na ucheleweshaji wa utekelezaji wa kazi za ujenzi wa barabara kwa visingizio vinavyotokana na mipangilio mibovu.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa niwajibu wa ngazi hizo za uongozi kuhakikisha kuwa kazi za barabara hazifanyiki kwa viwango duni na kukomesha uwepo wa upendeleo katika uteuzi wa wakandarasi wakazi za ujenzi wa barabara kinyume cha Sheria y aManunuzi.

Rais Kikwete akifungua Mkutano wa Nne wa Mwaka wa Maofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Bodi ya Mfuko wa Barabara na Wadau wa Barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa unao hudhuriwa na Wakuu wa Mikoa yote nchini na wilaya zote kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto, Arusha.

Rais Kikwete amewaambia viongozi hao kuwa kuondoa migongano ya maslahi kwa baadhi ya wataalam na viongozi wa halmashauri katika usimamizi wa barabara na kukomesha usimamizi duni katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.

Amewaambia washiriki wa mkutano huo: “Zipo changamoto za usimamizi zitokanazo na mapungufu katika ngazi ya Mkoa na Serikali za Mitaa ukiwemo ucheleweshaji wa utekelezaji wa kazi za ujenzi wa barabara kwa visingizio mbalimbali vitokanavyo na mipangilio mibovu na ujenzi wa barabara kwa viwango duni ikilinganishwa na viwango vilivyomo katika mikataba ya ujenzi wa barabarahizo.”

Mkutano huo unajadili barabara zinazo simamiwa na Serikali za Mitaa zikiwemo barabara za mijini na vijijini ambazo Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu sana ili kazi kubwa ya ujenzi wa barabara kuu iliyofanywa na uongozi wa Serikali ya sasa ya Awamu ya Nne ionekane ya maana. “Ipo pia changamoto ya kuteua makandarasi wakazi za barabara kwa upendeleo kinyume na Sheria ya Manunuzi na hivyo kupata wakandarasi wasio kuwa na uwezo na tuhuma kubwa za rushwa katika utoaji wa kazi za ujenzi wa barabara,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Changamoto nyingine ambazo nyie kama viongozi mnawajibu wa kukabiliana nazo ni pamoja na tuhuma za kuwepo kwa mgongano wa maslahi kwa baadhi ya wataalam na viongozi wa halmashauri mbalimbali nchini katika usimamizi wa kazi ya barabara na usimamizi duni wa ujenzi na matengenezo ya barabara zenyewe, wengine kwa uzembe na wengine kwa makusudi.”

Amesisitiza “Majawabu ya changamoto hizo yako ndani y amamlaka na uwezo wenu kuyatatua, maana yanatendeka mbele ya machoni penu na katika taasisi mnazo zisimamia. Ninawakumbusha na kuwasisitizia viongozi na watendaji wote wa halmashauri kutimiza wajibu wenu. Wajibu huo ndio sababu ya ninyi kuwemo katika nafasi za uongozi na utendaji mlizonazo.”