Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kuomboleza vifo vya askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan, vilivyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za vifo vya vijana wetu watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) ambao walikuwa wanalinda amani katika Darfur, Sudan ambavyo nimejulishwa kuwa vilitokea Jumapili iliyopita.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Vifo vya vijana wetu hawa vinasikitisha zaidi kwa kuzingatia kuwa wamepoteza maisha yao katika utumishi muhimu sana wa nchi yetu na katika kulinda amani ya Bara letu la Afrika. Tutaendelea kuwakumbuka kwa utumishi uliotukuka na mchango wao kwa nchi yetu na kwa Bara letu la Afrika.”
Amesema Mheshimiwa Rais Kikwete: “Kufuatia vifo hivyo, nakutumia wewe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi. Aidha, kupitia kwako, naomba uniwasilishie pole zangu nyingi kwa familia za vijana wetu ukiwajulisha kuwa moyo wangu uko nao wakati wa kipindi hiki kigumu cha kuwapoteza wapendwa wao. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke pema peponi roho za marehemu.”
Rais Kikwete pia amemtaka Jenerali Mwamunyange kuwafikishia salamu za pole Makamanda na askari wote wa Tanzania wanaolinda amani katika Darfur.
Askari hao wawili ambao ni sehemu ya wanajeshi 850 wa Tanzania wanaolinda amani katika Darfur na mwenzao mmoja ambaye hajulikani alipo mpaka sasa walipoteza maisha yao katika ajali ya gari lao kusombwa na maji wakati wakivuka mto katika Kijiji cha Hamada, eneo la Manawasha, Darfur.