RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa haiwezi kuitengenezea fitina Serikali ijayo kwa kuafiki kupandisha malipo ya posho ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopatiwa mikopo ya Serikali kutoka Sh. 7,500 za sasa hadi sh. 12,500 kwa siku.
Rais Kikwete ameyasema hayo Agosti 22, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Wanafunzi wa VyuoV ikuu Tanzania (Tahliso) Ikulu, Dar es salaam. Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wa Tahliso ambao ni pamoja na marais wa vyama vya wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini kuwa wakati Serikali yake inaingia madarakani, hali ya watoto waliokuwa wanamaliza shule ya msingi ilikuwa mbaya kiasi cha kwamba ni asilimia sita tu ya wanafunzi hao waliokuwa wanapata nafasi ya kuingia sekondari.
“Sasa tungefanya nini? Hali ilikuwa imefikia pabaya. Ilifikia kwamba wanafunzi waliokuwa wanapata nafasi ya kuingia sekondari walikuwa ni asilimia sita tu ya wanafunzi wote. Asilimia nyingine 94 ilikuwa inabakia nyumbani tu. Tulikuwa tunajenga taifa la watu wa shule ya msingi. Unapataje maendeleo katika hali hiyo, bila watu wenye elimu ya juu zaidi. Unajenga vipi tabaka katika jamii?” ameuliza Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amewambia viongozi hao wa wanafunzi kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kujenga vyuo vikuu vya Serikali katika kanda za Tanzania ambako kwa sasa hakuna vyuo vikuu. Maeneo kama kanda ya kusini na kanda nyingine ambazo zina vyuo vikuu lakini siyo vya Serikali.
Alisema kuwa ilikuwa lazima kuchukua hatua za haraka za kimapinduzi za kujenga shule za sekondari za kata nchini mwanzoni tu mwa uongozi wake kwa sababu kiwango cha watoto waliokuwa wanamaliza darasa la saba kuingia sekondari kilikuwa kimeshuka mno na kufikia asilimia sita tu kwa sababu ya ukosefu wa nafasi katika sekondari.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kujenga vyuo vikuu vya Serikali katika kanda ambazo kwa sasa hazina chuo hata kimoja kikuu katika kanda hizo. Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyok uwaeleza wanafunzi hao kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake, yakiwemo mafanikio katika sekta ya elimu.
“Hatujaweza, kwa mfano, kufanikiwa kufika mahali pa kutoa mikopo kwa wanafunzi wote nchini. Lakini tumepiga hatua kubwa. Wanafunzi wanaopatiwa mikopo ya elimu ya juu sasa wanakaribia wanafunzi 100,000 kutoka wanafunzi chini ya 10,000 mwaka 2005. Hata kiwango cha fedha za mikopo kimepanda kutoka sh.bilioni 40 hadi kufikia sh.bilioni 400 kwa sasa.”
Kuhusu maombi ya wanafunzi hao kutaka wanaopata mikopo ya Elimu ya Juu kupandishiwa kiwango cha posho ya kila siku kutoka sh. 7,500 hadi sh. 12,500, Rais Kikwete amesema:
“Nitazungumza na wale ambao wanatarajiwa kuongoza Serikali inayokuja. Kwenye hili, sitaki kuitengenezea fitina Serikali ijayo. Sitaki Serikali ijayo ianze kwa mgogoro wa mgomo wa wanafunzi hasa kama Serikali haitakuwa na uwezo wa kulipa kiwango hicho cha posho kwa sababu jambo hilo haliko kwenye Bajeti ya sasa. Ahadi kuhusu hili ni vizuri ikatolewa na wagombea urais katika kampeni za sasa. Mimi nimepandisha kiwango kutoka sh. 2,500 hadi sh. 5,000 hadi sh. 7,500 za sasa. Nawaomba kwa hili msubiri Rais ajaye.”
Wakati huo huo; Rais Kikwete Agosti 22, 2015, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Maalum wa Marekani katika Eneo la Maziwa Makuu, Bwana Thomas Perriello.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Bwana Perriello wamezungumzia hali ilivyo katika Eneo la Maziwa Makuu na hasa hali ya Burundi ambayo karibuni ilifanya Uchaguzi Mkuu ambako Rais Pierre Nkurunziza alifanikiwa kupata ushindi.
Wakati wa mazungumzo hayo, Bwana Perriello amepata nafasi ya kujitambulisha kwa Rais Kikwete kufuatia hatua ya karibuni ya Rais Barack Obama wa Marekani kumchagua kuwa Mwakilishi Maalum wa Marekani katika Eneo la Maziwa Makuu.
Rais Kikwete na mwakilishi huyo wa Marekani kimsingi wamekubaliana kuhusu jinsi gani ya kuisaidia Burundi kuleta hali ya maelewano na maridhiano kufuatia matukio ya karibuni ya kisiasa katika nchi hiyo jirani.
Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Bwana Perriello kwa uteuzi wake, akimtakia mafanikio katika kazi yake hiyo mpya na yenye changamoto nyingi na kubwa.
Bwana Perriello amempongeza Rais Kikwete na Tanzania kuhusu msimamo wake thabiti wa kibinadamu wa kupokea wakimbizi kutoka nchi jirani katika historia yote ya miaka 54 tokea uhuru wake.
“Mmeonyesha uongozi wa kutukuka kabisa katika suala hili la kupokea na kujali wakimbizi,” amesema Bw. Perriello ambaye alifuatana na Balozi wa Marekani katika Tanzania Bwana Mark Childress. Bwana Childress amekuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania tokea Mei 22, mwaka jana, 2014 alipowasilisha hati zake za utambuilisho kwa Rais Kikwete.
Bw. Perriello ana uzoefu mkubwa wa masuala ya Afrika kwasababu kabla ya uteuzi wake mwezi uliopita alifanyakazi na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) juu ya masuala ya amani na maridhiano katika Afrika.
Bw. Perriello ambaye alipata kuwa Mbunge wa Bunge la Wawakilishi wa Chama cha Democratic kutoka Jimbo la Virginia anachukua nafasi iliyoachwa wazi na seneta wa zamani Bwana Russ Fiengold, ambaye alimaliza muda wake Februari mwaka huu, 2015.
Bw. Perriello ambaye sasa atakuwa msimamizi mkuuu wa sera ya Marekani katika Eneo la Maziwa Makuu pia alishiriki katika kampeni ya Useneta ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana John Kerry mwaka 1996.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma kuhusu hali ya Sudan Kusini. Tanzania na Afrika Kusini zinashirikiana katika kuleta maridhiano ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha SPLM.