RAIS Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi amewaapisha wajumbe sita wa Tume ya Usuluhishi na uamuzi. Wajumbe walioapishwa ni Cornel Kananila Mtaki ambaye anakuwa Mwenyekiti wa tume hiyo ambapo makamisha ni Bibi Mary Cresent Massay, Bibi Salma Abdi Chande na Evod Paul Mushi.
Makamishna wenginei Sauli Herbet Kinemela na Yahya Kitambazi Msigwa. Wajumbe wa tume hii wanashika nafasi ya tume ya awali ambayo ilimaliza muda wao mapema mwaka 2011, ambapo wajumbe wa tume iliyoapishwa leo waliteuliwa mwishoni mwa mwaka 2011.
Wakati huo huo Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Viongozi wa Chama cha riadha nchini ambapo amewataka viongozi hao wafufue mchezo wa riadha hapa nchini.
“Kama kuna kitu mnataka serikali isaidie itawasaidia, lakini mchezo wa riadha kama michezo mingine, inahitaji juhudi za vilabu vya michezo yenyewe, na serikali inachangia tu lakini jukumu kubwa ni lenu.”. Rais amesema na kuwapa changamoto ya kuanza juhudi zao hizo katika ngazi za chini, ambapo ndipo wanapoweza kuvitambua vipaji vya watoto, kuvikuza na hatimaye kuviendeleza.
Rais amewakumbusha viongozi hao kuwa ahadi yake ya kusaidia michezo iko palepale, ambapo yuko tayari kugharamia wakufunzi au walimu wa michezo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukuza michezo hiyo hapa nchini.
Miaka ya nyuma, Tanzania ilikuwa inavunja rekodi mbalimbali duniani katika riadha kutokana na wanariadha wake ambao walikua mahiri na wenye viwango vikubwa duniani, lakini katika miaka ya hivi karibuni hali ni tofauti na juhudi za kuendeleza pale walipoishia hazijawahi kufanikiwa.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana na Michezo. Dk. Fenela Mukangara na Katibu Mkuu wa Wizara Sethi Kamuhanda. Rais amewataka viongozi hao wa riadha nchini kuwa wabunifu zaidi, kushirikisha wadau wengine wenye mapenzi na moyo na riadha, ili wapate kufikia malengo yao.