RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza viongozi nchini kuwaondoa mara moja watu wote waliovamia misitu na vyanzo vya maji, wakiwamo waliovamia Bonde la Mto Kilombero, Mkoani Morogoro. Rais Kikwete amesema kuwa kuanzia sasa viongozi wasiwaonee aibu watu wote wanaovamia misitu ya Serikali na kuharibu vyanzo vya maji na uoto wa asili.
“Viongozi tulisimamie hili bila woga wala aibu na wala wanasiasa wenzangu msiliingilie ili kupotosha watu. Kwenye hili, tusione haya wala aibu hata kidogo. Tuwaondoe wote na bila kuchelewa kwa sababu kwa kufanya hivyo tunanusuru taifa letu,” ameagiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alitoa maagizo hayo leo, Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipoweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Uboreshaji wa Upatikanaji Maji katika Mji wa Tabora kwenye siku ya tano na ya mwisho ya ziara yake Mkoani humo. Tokea Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete amekuwa katika Mkoa wa Tabora akikagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo zikiwamo barabara, miradi ya maji, shule na daraja.
Akizungumza na wananchi kwenye eneo la Bwawa la Igombe, nje ya Mji wa Tabora, Rais Kikwete amesema kuwa viongozi wakiendelea kuruhusu uvamizi wa maeneo ya misitu na vyanzo vya maji watakuwa wanaruhusu uangamizaji wa taifa.
“Hatuwezi kukubali jambo hilo, kila mtu ana kwao alikotokea, arudi kwao na siyo kuvamia misitu na mabonde katika maeneo mengine. Nawataka viongozi wahakikishe hili linafanyika bila woga wala haya. Waondoeni wavamizi wote katika mabonde, katika vyanzo vya maji na kwenye misitu.”
Rais amesema kuwa uamuzi wake aliochukua miezi mitatu tu baada ya kuingia madarakani wa kuwahamisha wafugaji waliokuwa wamevamia Bonde la Ihefu sasa umeanza kurudisha uhai kwenye Mto Ruaha. “ Watu waliingiza ng’ombe 460,000 katika eneo lile na kuharibu kabisa mfumo mzima wa Bonde lile. Tuliwaondoa na sasa angalau tunaanza kuona uhai kwenye Mto Ruaha ambao ulikuwa umekauka kwa sababu ya chanzo chake kuvurugwa na kuharibiwa.”
Rais amesema kuwa ni jambo la hatari kabisa kwa uhai wa binadamu kuharibu vyanzo vya maji kwa sbabau hakuna mbadala wa maji. “Tukikosa maji tutakunywa na kutumia nini? Soda? Unaweza kupika ugali kwa kutumia soda? Kinamama mnaweza kupiga ugali kwa kutumia soda?” Rais Kikwete amewauliza wananchi kwenye sherehe hiyo.