Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Pongezi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (T.E.C) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, kufuatia uteuzi uliofanywa na Baba Mtakatifu Francis, wa Padre Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Askofu Mteule Liberatus Sangu aliyekuwa Afisa katika Idara ya Uenezaji wa Injili kwa Mataifa katika Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, anatarajiwa kupewa Daraja la Uaskofu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga tarehe 12 Aprili, 2015.
“Nachukua fursa hii kukupongeza kwa dhati kabisa kwa mafanikio ambayo Kanisa Katoliki hapa nchini limeendelea kuyapata, kufuatia kuteuliwa kwa Padre Liberatus Sangu kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.
“Hii inadhihirisha wazi kutambuliwa kwa mchango mkubwa wa Padre Sangu katika kuwatumikia kikamilifu Kondoo wa Bwana hususan kupitia Idara nyeti ya Uenezaji wa Injili kwa Mataifa aliyokuwa akiitumikia akiwa Vatican ambako ndiyo Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani”, amesema Rais Kikwete katika pongezi zake.
Rais Kikwete amemuomba Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kumfikishia Salamu zake za Pongezi kwa Askofu Mteule Liberatus Sangu kwa kuteuliwa kwake, na amemtakia mafanikio zaidi katika Wadhifa wake Mpya wa Askofu katika kulitumikia Kanisa Katoliki na Waumini wa Kanisa hilo kwa ujumla hapa nchini, hususan katika Jimbo Katoliki la Shinyanga alikopangiwa kwenda kufanya kazi.