JK Atuma Salam za Rambirambi kwa Kenyatta

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuomboleza kifo cha Mjumbe wa Baraza la Seneti na Waziri muhimu wa zamani wa nchi hiyo, Mutula Kilonzo, aliyefariki dunia juzi, Ijumaa, mjini Nairobi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amemwambia Rais Kenyatta kuwa amepokea habari za kifo cha ghafla cha mwanasiasa huyo kwa mshtuko na huzuni na kuwa kifo chake kimeipokonya nchi hiyo mmoja wa viongozi waliokuwa wanajali na kutanguliza maslahi ya Kenya na wananchi wake.
“Kwa hakika, kifo cha Mheshimiwa Mutula Kilonzo kimeipokonya Kenya kiongozi muhimu. Mchango mkubwa aliuotoa katika kipindi cha kuivusha Kenya kutoka kwenye changamoto za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 hadi sasa ambako nchi imetulia na inasonga mbele, kamwe hautasahaulika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika nafasi zote za Uwaziri alizozishikilia katika kipindi hicho, kwanza kama Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba na baadaye kama Waziri wa Elimu, alijithibitisha na kujipambanua kama Mzalendo wa kweli kweli wa Kenya na mpenzi halisi wa nchi yake.”
Ameongeza Rais: “Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu zangu za rambirambi na zile za Serikali yangu kufuatia msiba huu. Aidha, kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu kwa familia ya Mheshimiwa Kilonzo. Nataka wajue kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na naungana nao kuomboleza na kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Mutula Kilonzo.Amin.”