Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Chifu Abdu Adam Mkwawa, ambaye aliaga dunia jana, Jumamosi, Februari 14, 2015 hospitalini mjini Iringa.
Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza Februari 15, 2015, Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na kushtushwa na kifo cha Chifu Mkwawa ambaye amemwelezea kama “Chifu mnzuri, kiongozi na mtu wa watu, ambaye katika maisha yake yote alihangaika kuenzi na kudumisha kumbukumbu za utamaduni wa Mkoa wa Iringa, za machifu wa mkoa huo na utalii wa Iringa.”
Rais Kikwete amemweleza Masenza: “Nawapeni pole sana na naungana nawe, familia ya marehemu na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa katika kuomboleza maisha ya Chifu na kiongozi ambaye tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake katika kujenga na kuendeleza mahusiano mazuri ndani ya jamii. Aidha, naungana na familia katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Abdu Adam Mkwawa. Amen.”
Wakati huo huo, kesho, Jumatatu, Februari 16, 2015, Rais Kikwete ataungana na wananchi wa Mkoa wa Iringa katika mazishi ya Marehemu Mkwawa.