JK Atuma Rambirambi Vifo vya Mvua ya Mawe Shinyanga

Rais Kikwete akizungumza

Rais Kikwete akizungumza


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,

Ali Nasoro Rufunga kuomboleza vifo vya watu 38 huku wengine 82 wakijeruhiwa usiku wa kuamkia tarehe 4 Machi, 2015.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika Kata ya Mwakata iliyoko katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali, hivyo kuathiri watu 3,500. katika Kata Mwakata iliyoathiriwa zaidi, kaya 350 zimeathiriwa katika Kijiji cha Makata wakati katika Kijiji cha Ngumbi, kaya 100 zimeathirika. Katika Kijiji cha Magung’hwa, kaya 50 zimeathiriwa..

“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 38 waliopoteza maisha na wengine 82 waliojeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huo.

Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa Wana-Shinyanga pekee bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.

“Naomba upokee Salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 38 kwa mara moja katika Mkoa wako. Kupitia kwako naomba Rambirambi zangu na Pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa, ndugu na jamaa zao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote Mahala Pema Peponi, Amina”, amezidi kuomboleza Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao, lakini amewataka wasisahau ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa. Aidha amewahakikishia wafiwa wote kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa Taifa.

“Namwomba Mola awawezeshe majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama kawaida”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.