RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Semamba Makinda kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Said Ramadhan Bwanamdogo. Said Ramadhan Bwanamdogo amefariki tarehe 22 Januari, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI) alikokuwa amelazwa akiendelea kupatiwa matibabu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Said Ramadhan Bwanamdogo, kilichotokea tarehe 22 Januari, 2014 akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Taasisi ya Mifupa (MOI) akiendelea na matibabu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza kifo cha Mbunge Bwanamdogo.
“Kwa hakika kifo cha Mbunge huyu ambacho kimenigusa mno, siyo tu ni pigo kubwa kwa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikokuwa akichangia kwa umahiri mijadala na hoja mbalimbali bali pia kwa Wananchi wa Jimbo la Chalinze ambao alikuwa akiwawakilisha vyema na kwa uhodari mkubwa katika Bunge hilo”, ameongeza kusema Rais Kikwete kwa masikitiko.
“Kufuatia taarifa za msiba huu, ninakutumia wewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda Salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Mbunge, Said Ramadhan Bwanamdogo”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Aidha Rais Kikwete amemuomba Spika Makinda kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu kwa kupotelewa na Baba, Kiongozi na Mhimili madhubuti wa familia ambaye kwa hakika alikuwa tegemeo kubwa kwao katika kuiendesha vyema familia yao. Hata hivyo amesema hawana budi kuutambua ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.
Amewahakikishia Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Said Ramadhan Bwanamdogo kuwa, katika msiba huu, hawako peke yao kwani yeye binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo na kwamba msiba huu ni wa wote. Amewaomba Wanafamilia kuwa wavumilivu, watulivu, wenye subira na ujasiri ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na Kiongozi na Mhimili wa familia. Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala pema Peponi Roho ya Marehemu Said Ramadhan Bwanamdogo, Amina.