RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameitumia salamu za rambirambi familia ya Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni la Rajani Group of Companies, Mzee Jayantilal Pragji Rajani kufuatia kifo cha mzee huyo kilichotokea Novemba 21, 2012, mjini London, Uingereza.
Katika salamu zake kwa familia hiyo, Rais Kikwete ameeleza masikitiko na huzuni yake kufuatia taarifa za kifo cha Mzee Rajani akimwelezea Mzee huyo kama mmoja wa watu waliochangia sana maendeleo ya nchi yetu kupitia shughuli za biashara, viwanda na mashirika ya kujitolea.
“Nilipata kumjua Mzee Jayantilal Pragji Rajani wakati wa maisha yake. Alikuwa mfanyabiashara mwenye bidii na aliyejituma sana katika maisha. Ni mmoja wa Watanzania wenzetu ambaye amechangia sana maendeleo ya nchi yetu kupitia shughuli za biashara, viwanda na Shirika la Kujitolea la Rotary. Tutamkumbuka kwa mchango wake huo katika maendeleo ya nchi yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nawatumieni salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa ambao taarifa zake nimezipokea kwa masikitiko na huzuni. Naelewa machungu mlinayo kwa kuondokewa na mhimili na mkuu wa familia yenu kwa miaka mingi. Naungana nanyi katika maombolezo. Aidha, namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki na naungana nanyi katika kumwomba aiweke pema peponi roho ya Marehemu Rajani. Amina.”