JK Atuma Rambirambi Kifo cha Jaji David Chipeta

Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mohamed Chande Othman

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mohamed Chande Othman kuomboleza kifo cha Jaji Buxton David Chipeta, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Jaji Mkuu Othman kuwa kifo cha Jaji Mstaafu Chipeta ni pigo kwa sababu bado ushauri wake ulikuwa unahitajika katika nyanja ya sheria na shughuli za Mahakama Tanzania.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu Chipeta ambaye nimejulishwa kuwa alipoteza maisha Jumanne mchana kwenye Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam. Tutamkumbuka Jaji Chipeta kama mtumishi mwaminifu na mwadilifu wa umma ambaye alifanya kazi zake kwa moyo wa kujituma katika kuhudumia jamii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katika nafasi zote alizopata kuzishikilia katika Mahakama tokea alipoajiriwa kwa mara ya kwanza Aprili 6, mwaka 1965, hadi kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 1978 na katika tume za uchunguzi ambako alishiriki, Jaji Chipeta alithibitisha utumishi uliotukuka na uadilifu mkubwa. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo wa utumishi bora na uadilifu katika jamii yetu.”

“Nakutumia wewe Mheshimiwa Jaji Mkuu salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu nikiomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako natuma salamu za rambirambi kwa Majaji wote wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kwa kuondokewa na mwenzao. Vile vile naomba unifikishie salamu zangu kwa watumishi wote wa Mahakama kwa kufikwa na msiba huu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Pia nakuomba unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa wanafamilia wote kwa kuondokewa na Babu, Baba na mhimili wa familia. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huo na naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Jaji Buxton David Chipeta. Amina.”