RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, kuomboleza kifo cha mtangazaji maarufu wa shirika hilo, Bi Halima Mohammed Mchuka ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Desemba 29, 2011 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
“Nimepokea kwa huzuni habari za kifo cha Halima Mohammed Mchuka. Nakutumia wewe Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo chake. Nakuomba, kupitia kwako, uniwasilishie salamu zangu kwa wafanyakazi wenzake katika TBC ambao wamempoteza mwenzao na rafiki yao.”
Ameongeza Rais katika salamu zake, “Aidha, nataka kupitia kwako niwatumie salamu zangu za rambirambi wana-familia, ndugu na jamaa wote za marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu wa maombolezo na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia.
Nawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amen.”
Rais pia amesema kuwa Bi. Mchuka ametoa mchango mkubwa katika nyanja ya utangazaji nchini. “Sote tutaendelea kukumbuka weledi wake, uzalendo wake na ujasiri wake katika utangazaji uliomsukuma kuwa Mwanamke wa Kwanza katika Tanzania kutangaza mechi za mpira wa miguu”.
Ameongeza Rais Kikwete: “Ni dhahiri kuwa nyanja ya utangazaji imeondokewa na mtu muhimu na namna nzuri zaidi ya kumuenzi Bi. Mchuka ni kwa watangazaji waliobakia kuendelea kuiga mfano wake katika ubora wa utangazaji nchini mwetu.”
Mtangazaji huyo wa kike mahiri aliyetokea hata kumudu kutangaza soka amefariki dunia baada ya kupata tatizo la kiharusi jana akiwa kazini. Taarifa zinasema tatizo hilo lilishawahi kumpata mwaka 2007 Januari na kulazwa hospitalini.
Halima Mchuka alijiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam miaka ya 1990 na kuondokea kuwa maarufu katika michezo hasa utangazaji wa mpira uwanjani.